By:Hassan Pojjo

Viongozi wa ukanda wa Pwani, wakiongozwa na Mbunge wa Jomvu Badi Twalib, wametoa wito kwa wanasiasa nchini kuwa waangalifu na matamshi yao kuhusu sekta ya utalii, wakionya kuwa kauli zinazoweza kuwakatisha tamaa watalii kutembelea Kenya zina athari kubwa kwa uchumi na maisha ya maelfu ya wananchi.
Akizungumza kwa niaba ya viongozi wa Pwani, Badi alisema sekta ya utalii ndiyo mhimili wa uchumi katika eneo hilo, ikitoa ajira na kipato kwa maelfu ya watu wakiwemo wafanyakazi wa hoteli, waongoza watalii, wafanyabiashara wadogo, wavuvi, wasanii wa kazi za mikono na madereva wa usafiri wa watalii.

Alisema viongozi wa Pwani wameungana kulaani kauli zozote zinazoweza kuharibu taswira ya Kenya kama moja ya mataifa yanayoongoza kwa utalii barani Afrika, akisisitiza kuwa tofauti za kisiasa hazipaswi kutangulizwa mbele ya maslahi ya wananchi.
“Tofauti za kisiasa ni sehemu ya demokrasia, lakini hazipaswi kuhatarisha uchumi wa wananchi au kuharibu sifa ya Kenya katika jukwaa la kimataifa,” alisema.
Viongozi hao wamewahakikishia watalii wa ndani na wa kimataifa kuwa ukanda wa Pwani unaendelea kuwa salama, wenye utulivu na tayari kuwapokea wageni kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Pia wametoa wito kwa viongozi wa kisiasa, sekta binafsi na wananchi kushirikiana kulinda taswira ya Kenya na kuendeleza sekta ya utalii, ambayo ni miongoni mwa nguzo kuu za uchumi wa taifa kupitia mapato ya fedha za kigeni na utoaji wa ajira.
Kauli hiyo inajiri wakati kukiwa na mjadala kuhusu athari za matamshi ya kisiasa kwa taswira ya Kenya kimataifa, huku viongozi wa Pwani wakisisitiza kuwa kulinda hadhi ya sekta ya utalii ni muhimu kwa ustawi wa uchumi wa taifa na maisha ya wananchi wanaoutegemea.
