By:Alii Vincent

Baadhi ya wafuasi wa Chama cha ODM katika Kaunti ya Kwale wamekihama chama hicho na kujiunga na mrengo wa Linda Mwananchi unaoongozwa na Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna.
Miongoni mwa walioasi mrengo wa Chungwa ni Ginorah Kinyasi, ambaye amesema wameamua kujiondoa ODM kwa madai kuwa chama hicho hakina mwelekeo wa kuongoza taifa. Amewataka wakazi wa Kwale kuunga mkono mrengo wa Linda Mwananchi.
Kwa upande wao, Bijuma N’kale, anayewania nafasi ya Mwakilishi wa Wanawake wa Kwale kwa tiketi ya Linda Mwananchi, na Abdalla Mambo, aliyewahi kuwa mwenyekiti wa ODM katika eneo bunge la Msambweni, wamesema mabadiliko ya uongozi nchini yanahitaji wananchi kufanya maamuzi mapya katika nyadhifa mbalimbali za uongozi.
Wawili hao pia wamesisitiza kuwa uongozi bora unapaswa kuzingatia na kulinda maslahi ya wananchi wote bila ubaguzi.
Kauli hizo zilitolewa wakati wa mkutano na wanahabari uliofanyika katika Uwanja wa Maonyesho wa Ukunda, Kaunti ya Kwale.
