By:Hassan Pojjo

: Serikali ya Kaunti ya Mombasa imeanzisha mikakati mipya ya kuboresha usimamizi wa masoko ya umma na kuimarisha mazingira ya biashara, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wafanyabiashara na wananchi.
Hatua hiyo ilijadiliwa katika kikao cha mashauriano kilichowakutanisha wasimamizi wa masoko (Market Masters) kutoka maeneo mbalimbali ya kaunti, kikiongozwa na Afisa Mkuu wa Biashara Khamis Juma Kurichwa kwa kushirikiana na Waziri wa Biashara wa Kaunti Mohamed Osman Ali.

Mkutano huo ulijadili changamoto zinazokabili masoko ya umma, ikiwemo usimamizi, utoaji wa huduma na mazingira ya biashara, huku ukiweka mikakati ya kuimarisha uwajibikaji na kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa masoko.
Akizungumza baada ya kikao hicho, Kurichwa alisema wasimamizi wa masoko wana nafasi muhimu katika kuhakikisha masoko yanaendeshwa kwa utaratibu, usafi na ufanisi, huku yakikidhi mahitaji ya wafanyabiashara na wananchi.
Alisema serikali ya kaunti itaendelea kushirikiana kwa karibu na wasimamizi hao ili kutatua changamoto zinazojitokeza na kuhakikisha huduma katika masoko zinaimarika.

Kwa upande wake, Waziri wa Biashara Mohamed Osman Ali alisema kuboresha mazingira ya biashara ni hatua muhimu katika kukuza uchumi wa Mombasa na kuongeza fursa kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati.
Aliongeza kuwa serikali ya kaunti itaendelea kuimarisha usimamizi wa masoko kupitia mashauriano ya mara kwa mara na wadau mbalimbali, ili kuhakikisha masoko yanakuwa salama, yenye utaratibu na yanachangia ukuaji wa uchumi wa eneo hilo.
Viongozi hao walisema hatua hiyo inaendana na ajenda ya maendeleo ya Serikali ya Kaunti ya Mombasa ya kuboresha utoaji wa huduma za umma, kuongeza uwajibikaji katika idara za serikali na kuimarisha mazingira ya biashara katika masoko ya umma.
