By:Athuman Luchi

Serikali imesema ujenzi wa Bwawa la Mwache katika Kaunti ya Kwale umefikia asilimia 90, huku hatua za mwisho zikikamilishwa kabla ya kuanza kwa uhifadhi wa maji ifikapo Oktoba mosi mwaka huu.
Waziri wa Maji, Usafi wa Mazingira na Umwagiliaji, Eric Mugaa, amesema ujenzi wa ukuta mkuu wa bwawa hilo umefikia hatua ya juu, na serikali iko tayari kuanza kujaza bwawa maji baada ya kuhakikisha miundombinu yote muhimu imekamilika.
Bwawa hilo lina uwezo wa kuhifadhi hadi lita bilioni 136 za maji, huku kiwanda cha kusafisha maji kikitarajiwa kuzalisha hadi lita milioni 186 kwa siku kwa ajili ya wakazi wa Mombasa na Kwale.
Serikali pia imetenga shilingi bilioni 13.6 kuhakikisha mradi huo unakamilika kikamilifu.
Aidha, ujenzi wa bwawa dogo la kuzuia mchanga umefikia asilimia 87, huku kandarasi za mabomba ya kusambaza maji katika maeneo ya South Coast na North Coast tayari zimetolewa.
Waziri Mugaa amesema ujenzi wa kiwanda cha kusafisha maji utaanza rasmi katikati ya Septemba.

Wakati huo huo, serikali imesema inaendelea kusaidia familia zilizoathiriwa na ujenzi wa bwawa hilo, ikiwemo ujenzi wa shule, vituo vya ECDE na kuwapatia wananchi vifaa vya kuanzisha biashara na shughuli za kujipatia kipato.
Serikali inalenga kuhakikisha Bwawa la Mwache linakuwa chanzo muhimu cha maji kwa zaidi ya wakazi milioni moja na nusu katika maeneo ya Mombasa na Kwale, na kusaidia kukuza afya, kilimo na shughuli za kiuchumi katika Pwani.
