By:Hassan Pojjo

Serikali ya Tanzania imetangaza mpango wa kusambaza gesi asilia kwenda Kenya na Uganda kupitia miundombinu ya bomba moja, hatua inayotarajiwa kuimarisha ushirikiano wa kikanda, kuongeza matumizi ya nishati safi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika Ukanda wa Afrika Mashariki.
Kauli hiyo imetolewa wakati wa Kongamano la Pili la Kimataifa la Vijana wa Afrika kuhusu Mafuta na Gesi linaloendelea mjini Unguja.
Tanzania imeeleza kuwa inaendelea na maandalizi ya utekelezaji wa mradi wa kusambaza gesi asilia kwenda Kenya na Uganda kupitia bomba moja la gesi, mradi unaolenga kuunganisha nchi za Afrika Mashariki katika matumizi ya nishati safi na salama kwa mazingira.
Akizungumza katika Kongamano la Pili la Kimataifa la Vijana wa Afrika kuhusu Mafuta na Gesi linalofanyika mjini Unguja,
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Mhandisi Charles Sangweni, amesema mpango huo ni sehemu ya mkakati wa Tanzania wa kuimarisha uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi na kuhakikisha rasilimali hizo zinawanufaisha wananchi wa Tanzania pamoja na mataifa jirani.
Sangweni amesema kuwa maendeleo ya miundombinu ya gesi yataongeza biashara ya kikanda, kuimarisha usalama wa nishati na kusaidia nchi za Afrika Mashariki kupunguza utegemezi wa nishati zinazochafua mazingira.
Aidha, amesema kongamano hilo limewaleta pamoja viongozi wa serikali, wawekezaji, wataalamu wa sekta ya mafuta na gesi, taasisi za elimu pamoja na vijana kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika kwa lengo la kujadili namna ya kuongeza uwekezaji, kukuza matumizi ya nishati safi na kuimarisha ushiriki wa vijana katika sekta hiyo muhimu.
Kwa mujibu wa Sangweni, vijana wanapaswa kupewa nafasi kubwa zaidi kupitia mafunzo, ubunifu na ajira ili waweze kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya sekta ya mafuta na gesi, ambayo ina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa mataifa ya Afrika.
Washiriki wa kongamano hilo pia wamejadili matumizi ya teknolojia za kisasa, uendelezaji wa rasilimali za mafuta na gesi kwa njia endelevu, pamoja na umuhimu wa ushirikiano wa kikanda katika kufanikisha miradi mikubwa ya nishati.
Mpango wa Tanzania wa kusambaza gesi kupitia bomba moja kwenda Kenya na Uganda unatarajiwa kufungua fursa mpya za uwekezaji, kuongeza upatikanaji wa nishati kwa viwanda na matumizi ya nyumbani, huku ukiimarisha uhusiano wa kiuchumi na maendeleo ya pamoja katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Wadau wa sekta ya nishati wanaamini kuwa utekelezaji wa mradi huo utaifanya Afrika Mashariki kuwa kitovu muhimu cha biashara ya gesi asilia, huku ukitoa fursa zaidi kwa vijana na wawekezaji kushiriki katika maendeleo ya sekta ya mafuta na gesi barani Afrika.
