Share this to

By:Hassan Pojjo

Wafanyabiashara wa Soko la Kongowea Ndogo, Kaunti ya Mombasa, wametaka kushirikishwa kikamilifu katika utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa soko la kisasa unaofadhiliwa na Serikali ya Kitaifa kwa gharama ya shilingi milioni 70.

Wakizungumza katika kikao cha mashauriano kilichoongozwa na Mbunge wa Jomvu, Badi Twalib, wafanyabiashara hao walisema wanakaribisha maendeleo lakini wanataka kuwepo kwa mpango wa wazi utakaolinda biashara zao na kuhakikisha hakuna mfanyabiashara atakayepoteza chanzo chake cha mapato wakati wa utekelezaji wa mradi huo.

Kwa mujibu wa wawakilishi wa wafanyabiashara, zaidi ya familia 2,000 zinategemea Soko la Kongowea Ndogo kwa riziki, hivyo walisisitiza umuhimu wa mazungumzo ya kina kabla ya ujenzi kuanza.

Mradi huo ni sehemu ya mpango wa Serikali ya Kitaifa wa Modern Markets Programme, unaolenga kuboresha masoko ya umma kwa kujenga miundombinu ya kisasa, salama na rafiki kwa wafanyabiashara pamoja na wateja.

Akizungumza baada ya mkutano huo, Mbunge wa Jomvu Badi Twalib alisema utekelezaji wa mradi huo utazingatia maoni ya wananchi kupitia mchakato wa ushirikishwaji wa umma, akisisitiza kuwa maendeleo yanapaswa kwenda sambamba na kulinda maslahi ya wananchi.

Aliongeza kuwa kutafanyika mikutano zaidi itakayowaleta pamoja wafanyabiashara, viongozi wa soko na wadau wengine ili kufikia mwafaka kuhusu namna bora ya kutekeleza mradi huo.

Mbunge huyo aliwahakikishia wafanyabiashara kuwa hakuna atakayebaguliwa au kuathiriwa bila kusikilizwa, akisema lengo la ujenzi wa soko hilo ni kuboresha mazingira ya biashara, kuongeza usalama, usafi na kuimarisha shughuli za kiuchumi katika Jomvu na maeneo ya jirani.

Wafanyabiashara walieleza matumaini kuwa kupitia mazungumzo hayo, mradi huo utatekelezwa kwa uwazi na kwa njia itakayowezesha maendeleo huku ukihifadhi ajira na vyanzo vya mapato vya maelfu ya wananchi.


Share this to

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *