Share this to

By:Farida Ali

Serikali imeongeza juhudi za kuimarisha usalama kuanzia ngazi ya kijiji, kukabiliana na biashara ya dawa za kulevya, na kuhakikisha wananchi wanaostahili wanapata vitambulisho vya kitaifa kwa urahisi.

Hatua hiyo inajiri huku maafisa wa Utawala wa Serikali Kuu (NGAOs) wakitakiwa kuongeza juhudi katika kutekeleza majukumu yao na kuimarisha ushirikiano na vyombo vya usalama.

Akizungumza katika mkutano na Maafisa wa Utawala wa Serikali Kuu Kaunti ya Mombasa, Katibu Mkuu wa Usalama wa Ndani na Utawala wa Kitaifa, Dkt. Raymond Omollo, alisema usalama wa Mombasa ni msingi muhimu wa uchumi wa taifa kutokana na nafasi ya kaunti hiyo kama lango kuu la biashara kupitia Bandari ya Mombasa.

Alisema kuwa amani na utulivu wa Mombasa vina mchango mkubwa katika kukuza biashara, utalii na uwekezaji nchini.

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Kamishna wa Kanda ya Pwani Paul Rotich pamoja na Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Mohammed Hassan. Dkt. Omollo aliwataka makamishna wa kaunti, machifu, manaibu wao na wazee wa Nyumba Kumi kushirikiana kwa karibu na mashirika ya usalama pamoja na wananchi ili kukabiliana na uhalifu.

Alisisitiza kuwa juhudi hizo zinalenga kusambaratisha makundi ya uhalifu, kupambana na misimamo mikali ya kidini, na hasa kudhibiti biashara ya dawa za kulevya ambayo imeendelea kuwa tishio kwa vijana. Aidha, alisema mapambano dhidi ya dawa za kulevya ni jukumu la kila mdau, wakiwemo wazazi, viongozi wa dini, mahakama na vyombo vya usalama.

Katika sekta ya afya, Dkt. Omollo aliipongeza Kaunti ya Mombasa kwa kufikia asilimia 83 ya usajili wa Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA), hatua iliyoifanya kuwa miongoni mwa kaunti zinazoongoza nchini.

Kuhusu utoaji wa vitambulisho vya kitaifa, aliwataka maafisa wa utawala kuhakikisha hakuna Mkenya anayenyimwa fursa ya kupata kitambulisho cha kitaifa, akibainisha kuwa nyaraka hiyo ni muhimu katika kupata elimu, ajira, huduma za kifedha na kufurahia haki za kidemokrasia.

Akihitimisha hotuba yake, Dkt. Omollo aliwahakikishia maafisa hao kuwa Serikali Kuu itaendelea kuwapa ushirikiano na rasilimali kupitia Ajenda ya BETA ili kuimarisha utoaji wa huduma na kudumisha amani kuanzia ngazi ya kijiji.


Share this to

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *