By:Alii Vincent

Idara ya Afya katika Kaunti ya Kilifi inaendelea na kampeni ya siku 10 ya utoaji chanjo dhidi ya ugonjwa wa Mpox, huku ikiongeza juhudi za kudhibiti kuenea kwa maambukizi baada ya visa 38 na kifo kimoja kuripotiwa kaunti hiyo.
Kampeni hiyo iliyoanza rasmi Ijumaa iliyopita inalenga zaidi maeneo bunge ya Kaloleni na Rabai, ambayo yamebainika kuwa na idadi kubwa ya maambukizi.
Akizungumza baada ya mkutano wa wadau uliofanyika Kaloleni, Afisa Mkuu wa Huduma za Matibabu katika Kaunti ya Kilifi, Dkt. Saumu Chufi, alisema kuwa kati ya visa 38 vilivyorekodiwa, vinane vimetokea Kaloleni, eneo ambalo pia limeripoti kifo kimoja kutokana na ugonjwa huo.
Kwa upande wake, Naibu Kamishna wa Kaloleni, Jasmine Musembi, amewataka wakazi kushirikiana kikamilifu na wahudumu wa afya ili kuhakikisha kampeni ya chanjo inafanikiwa na kusaidia kudhibiti maambukizi mapya.
Ili kuongeza ufanisi wa zoezi hilo, idara ya afya imeweka mkazo katika kuwafikia watu walio katika hatari kubwa ya kuambukizwa, wakiwemo madereva wa magari ya masafa marefu, wahudumu wa afya walioko mstari wa mbele, pamoja na wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao katika vituo vikuu vya biashara na maeneo ya mipakani.
Maafisa wa afya wamewahimiza wananchi kujitokeza kupokea chanjo, kuendelea kuzingatia kanuni za usafi binafsi, na kuripoti mapema katika vituo vya afya endapo watapata dalili zinazohusishwa na ugonjwa wa Mpox.
