By:Farida Ali

Wakazi wa Kibarani katika Kaunti ya Mombasa wanatarajiwa kunufaika na miradi mipya ya elimu na miundombinu iliyozinduliwa ili kuboresha huduma za kijamii na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika eneo hilo.
Miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa jengo jipya la utawala katika Shule ya Kibarani Comprehensive School, ambalo linatarajiwa kuboresha mazingira ya kazi kwa walimu na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa shule.

Aidha, viongozi walizindua rasmi mradi wa ujenzi wa Barabara ya Kibarani Ring Road, unaotarajiwa kurahisisha usafiri, kuimarisha mawasiliano kati ya maeneo mbalimbali na kufungua fursa zaidi za biashara na uwekezaji.
Hafla ya uwekaji wa mawe ya msingi ilihudhuriwa na Gavana wa Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir, Mbunge wa Jomvu Badi Twalib pamoja na viongozi wengine wa eneo hilo, ambao waliwahimiza wananchi kuendelea kuunga mkono miradi ya maendeleo.

Viongozi hao walisema uwekezaji katika elimu na miundombinu ni nguzo muhimu katika kuinua uchumi wa eneo na kuboresha maisha ya wananchi, huku wakisisitiza kuwa ushirikiano kati ya serikali na wananchi ni muhimu ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kuwanufaisha wakazi.
