By:Alii Vincent

Wafanyabiashara wadogo katika Kaunti ya Mombasa wanatarajiwa kunufaika baada ya Mamlaka ya Barabara Kuu nchini (KeNHA) kukabidhi rasmi Soko la Kisasa la Mikindani kwa Serikali ya Kaunti ya Mombasa ili kuanza kutumika.

Soko hilo, lenye uwezo wa kuhudumia zaidi ya wafanyabiashara 170, lilikabidhiwa na Mkurugenzi Mkuu wa KeNHA, Injinia Luka Kipchumba Kimeli, katika hafla iliyohudhuriwa na Gavana wa Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir, Mbunge wa Jomvu Badi Twalib na viongozi wengine.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mbunge wa Jomvu Badi Twalib alisema soko hilo litachochea biashara na kuinua uchumi wa wakazi wa Jomvu na Changamwe, huku likiwapa wafanyabiashara mazingira bora na salama ya kuendesha shughuli zao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa KeNHA Luka Kipchumba Kimeli alisema ujenzi wa soko hilo ni sehemu ya mradi wa upanuzi wa Barabara Kuu ya Mombasa–Mariakani. Alisema soko hilo limejengwa kuwafidia na kurejesha shughuli za kiuchumi za wafanyabiashara walioathiriwa na upanuzi wa barabara hiyo.

Baada ya kukabidhiwa kwa mradi huo, Serikali ya Kaunti ya Mombasa sasa itasimamia uendeshaji wa soko hilo na kuhakikisha wafanyabiashara wanapata mazingira bora ya kufanya biashara.

Viongozi waliohudhuria hafla hiyo waliipongeza KeNHA pamoja na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa kufadhili mradi huo, wakisema uwekezaji katika miundombinu unapaswa kuwanufaisha wananchi kwa kuongeza fursa za biashara, ajira na ukuaji wa uchumi.

