Share this to

Muungano wa Wauguzi na Wakunga nchini (KNUNM) umetoa notisi ya siku saba ya mgomo, ukisema wanachama wake wataacha kutoa huduma katika hospitali zote za kaunti endapo serikali haitatekeleza matakwa yao.

Miongoni mwa madai ya muungano huo ni kuajiri kwa masharti ya kudumu na ya pensheni wahudumu wa Mpango wa Afya kwa Wote (UHC), kushughulikia kucheleweshwa kwa kupandishwa vyeo, kusainiwa kwa Mkataba mpya wa Makubaliano ya Pamoja ya Ajira (CBA), pamoja na kutekelezwa kwa makubaliano ya awali kati ya serikali na wafanyakazi.

Tangazo hilo linajiri huku maelfu ya wahudumu wa UHC wakiendelea na mgomo wao, hali inayoongeza presha kwa serikali ya kitaifa na zile za kaunti kuhusu nani anayepaswa kuajiri na kugharamia mishahara ya wafanyakazi hao.

Katika barua walizozielekeza kwa Mawaziri wa Afya na Utumishi wa Umma, Baraza la Magavana, Tume ya Utumishi wa Umma pamoja na Tume ya Mishahara na Marupurupu, viongozi wa KNUNM wamesema serikali imepuuza malalamishi ya wauguzi licha ya mazungumzo ya mara kwa mara.

Muungano huo unataka wahudumu wote wa UHC waajiriwe kwa masharti ya kudumu na kubaki kwenye mfumo wa malipo wa serikali ya kitaifa badala ya kuhamishiwa serikali za kaunti.

Aidha, KNUNM imeeleza kuwa kaunti zote 47 bado hazijapokea fedha za mishahara ya wafanyakazi hao, licha ya Hazina ya Taifa kutenga shilingi bilioni 8.6 kwa ajili ya kuwaajiri rasmi na Wizara ya Afya kueleza kuwa mchakato wa uhamisho ulikuwa umekamilika.


Share this to

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *