By:Hassan Pojjo

Kiongozi wa kisiasa wa Wadi ya Kisurutini, Ndune Munga, ameendelea kuonyesha dhamira yake ya kuwekeza katika maendeleo ya vijana kupitia michezo, akisisitiza kuwa soka ni moja ya nyenzo muhimu za kuwawezesha vijana kiuchumi na kijamii.
Akizungumza baada ya kukabidhi mipira kwa baadhi ya timu za soka za eneo hilo, Ndune alisema ataendelea kusimama pamoja na vijana wa Kisurutini kwa kuhakikisha wanapata mazingira bora ya kukuza vipaji vyao na kushiriki mashindano mbalimbali.

Katika hatua ya kuunga mkono timu hizo, Ndune amekabidhi mipira kwa timu za Rabai Sports FC na Kingstarz FC, huku akitangaza kuwa siku ya Jumatatu atatembelea FC Uwanja kwa lengo la kukutana na wachezaji na viongozi wa timu hiyo pamoja na kuwapa msaada wa vifaa vya michezo.
Alisema uwekezaji katika michezo ni uwekezaji wa moja kwa moja kwa vijana, kwani unawapa nafasi ya kuonyesha vipaji vyao, kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya pamoja na vitendo vya uhalifu.
Ndune alieleza kuwa ana maono ya kuifanya Kisurutini kuwa kitovu cha vipaji vya soka katika Kaunti ya Kilifi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa michezo ili vijana wapate nafasi ya kuonekana na vilabu vikubwa nchini na hata nje ya nchi.

Aidha, aliahidi kuwa endapo wananchi watampa nafasi ya kuwa Mjumbe wa Bunge la Kaunti (MCA) wa Wadi ya Kisurutini katika uchaguzi ujao, ataweka utaratibu wa kuhakikisha timu zote za soka katika wadi hiyo zinapata msaada wa mara kwa mara wa mipira, jezi na vifaa vingine muhimu vya michezo.
“Malengo yangu ni kuona kila kijana mwenye kipaji anapata fursa ya kukiendeleza. Michezo ni njia ya kuleta maendeleo, ajira na umoja katika jamii yetu.
Nikiwa MCA, hakuna timu itakayosahaulika kwani nitahakikisha zinapata mipira na jezi kila wakati,” alisema Ndune.

Viongozi wa timu zilizopokea msaada huo walimshukuru kwa hatua hiyo wakisema imekuja wakati mwafaka ambapo vilabu vingi vya mashinani vinakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vifaa vya michezo.
Walieleza kuwa msaada huo utawapa motisha wachezaji na kuongeza ushindani katika ligi na mashindano mbalimbali ya eneo hilo.
Hatua hiyo imepokelewa vyema na vijana wa Kisurutini, wengi wakisema ushirikiano kati ya viongozi na sekta ya michezo unaweza kuwa chachu ya kuibua vipaji vipya na kufungua fursa zaidi za maendeleo kwa vijana wa eneo la Rabai na Kisurutini kwa ujumla.
