By:Hassan Pojjo

Kipa chipukizi mwenye umri wa miaka 19, Mwayaga Junior, ametoa wito kwa akademia za soka, vilabu na wadau wa mchezo huo kumpa nafasi ya kuonyesha uwezo wake huku akisaka fursa ya kuendeleza kipaji chake.
Mwayaga amesema ndoto yake ni kujiunga na akademia yenye mazingira bora ya mafunzo ili kuboresha kiwango chake na hatimaye kucheza katika ligi za ushindani nchini na kimataifa.
Ameeleza kuwa ana nidhamu, ari ya kujifunza na kujituma, akiamini kuwa sifa hizo zitamwezesha kufikia ndoto yake ya kuwa miongoni mwa makipa bora siku zijazo.
Kipa huyo amewaomba makocha, viongozi wa vilabu, wasimamizi wa akademia na mawakala wa vipaji kumpa nafasi ya kufanya majaribio, akisema ana imani uwezo wake utaonekana atakapopata fursa ya kucheza.
Aidha, amewahimiza wadau wa soka kuendelea kuwekeza katika ukuzaji wa vipaji vya vijana kupitia akademia na programu za maendeleo, akisema hatua hiyo itasaidia kuibua kizazi kipya cha wachezaji wenye uwezo wa kushindana katika viwango vya juu.
Mwayaga amesema ana matumaini kuwa kupitia ushirikiano wa jamii ya soka, atapata fursa ya kujiunga na akademia itakayomwezesha kuendeleza kipaji chake na kutimiza ndoto yake ya kuwa kipa wa kulipwa.
