Share this to

By:Glory Mwagambo

Walimu wanaofunza wanafunzi wenye ulemavu katika Shule ya Sir Ali Special mjini Malindi, Kaunti ya Kilifi, wameitaka serikali pamoja na wadau mbalimbali kuongeza usaidizi kwa shule hiyo ili kukabiliana na changamoto zinazowakabili wanafunzi na walimu.

Walimu hao wamesema licha ya kuwepo kwa maendeleo katika kutambua haki za watu wenye ulemavu, bado kuna changamoto kubwa zinazohitaji kushughulikiwa, ikiwemo uhaba wa rasilimali za masomo, chakula na miundombinu shuleni.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sir Ali Special, Agnes Kwekwe, amesema amekuwa akihudumu katika shule za wanafunzi wenye ulemavu tangu mwaka 2009, na ameshuhudia mabadiliko makubwa katika namna jamii inavyowatambua watu wenye ulemavu.

Hata hivyo, amesema bado haki za watu hao hazijazingatiwa kikamilifu, akibainisha kuwa baadhi ya changamoto huanzia katika familia ambapo baadhi ya wazazi hawapi kipaumbele elimu ya watoto wao wenye ulemavu.

Kwekwe amesema baadhi ya wazazi huona kuwasomesha watoto hao kuwa ni kupoteza fedha, hali inayosababisha baadhi yao kubaki majumbani bila kupata elimu inayostahili.

Amesema shule hiyo pia inakabiliwa na uhaba wa chakula, madarasa, vitanda na vifaa vingine muhimu, huku msaada unaopatikana kutoka kwa serikali ukiwa hautoshelezi mahitaji yaliyopo.

Kwa mujibu wake, changamoto ya chakula imekuwa kubwa kiasi kwamba wakati mwingine shule hulazimika kufunga mapema kabla ya muhula kumalizika rasmi.

Aidha, Kwekwe amesema walimu hukumbana na wakati mgumu kuwafundisha baadhi ya wanafunzi kutokana na ukosefu wa malezi na mafunzo ya nidhamu kutoka nyumbani, hali inayoongeza ugumu katika mchakato wa elimu.

Ameongeza kuwa watu wenye ulemavu bado wanakumbana na ubaguzi katika jamii, jambo linalowalazimu kuunda vikundi vya kujisaidia ili kupata msaada kutoka kwa wahisani mbalimbali.

Kwekwe ameitaka jamii kutambua kuwa watu wenye ulemavu ni sehemu muhimu ya jamii na wana vipaji mbalimbali vinavyoweza kuchangia maendeleo ya taifa, hivyo wanapaswa kupewa fursa sawa bila kubaguliwa.


Share this to

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *