Share this to

By:Farida Ali

Serikali imesitisha mara moja shughuli zote za uchimbaji madini zinazofanywa na kampuni ya Tata Chemicals Magadi Limited hadi itakapotekeleza kikamilifu masharti ya Sheria ya Madini na kanuni nyingine zote zinazosimamia sekta hiyo nchini.

Voiced Package

Uamuzi huo ulitangazwa na Waziri wa Madini, Uchumi wa Buluu na Masuala ya Bahari, Hassan Ali Joho, kufuatia kile alichosema ni kutotekelezwa kwa majukumu muhimu ya kisheria licha ya mazungumzo ya muda mrefu kati ya serikali na kampuni hiyo.

Kwa mujibu wa wizara, kampuni hiyo imebainika kuwa na mapungufu kadhaa ikiwemo kukosa mpango wa kuongeza thamani ya madini nchini, kutokamilisha upatanisho na malipo ya mirahaba ya madini, udhaifu katika utoaji wa taarifa za mauzo ya madini nje ya nchi, utekelezaji hafifu wa Makubaliano ya Maendeleo ya Jamii (CDA), pamoja na ukosefu wa mpango wa kuwaajiri na kuwajengea uwezo Wakenya.

Aidha, wizara imeeleza kuwa kampuni hiyo haijazingatia ipasavyo matumizi ya bidhaa na huduma za ndani na imeonyesha mapungufu katika utekelezaji wa masharti ya uhifadhi wa mazingira.

Kutokana na hali hiyo, Tata Chemicals Magadi Limited imeagizwa kuwasilisha nyaraka na ushahidi unaothibitisha kuwa imetimiza kikamilifu wajibu wake wa kisheria na kushughulikia madeni au majukumu yote yaliyosalia kabla ya kuruhusiwa kurejea katika shughuli za uchimbaji madini.

Waziri Joho amesema serikali itaendelea kusimamia sekta ya madini kwa kuhakikisha rasilimali za taifa zinatumika kwa uwajibikaji, kwa njia endelevu na kwa manufaa ya uchumi wa nchi, huku mazingira yakilindwa na maslahi ya jamii zinazoishi katika maeneo ya uchimbaji yakipewa kipaumbele.


Share this to

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *