Share this to

By:Alii Vincent

Mashindano ya kimataifa ya baiskeli ya LOOP Safari Gravel Series yatarejea nchini baadaye mwezi huu kwa mchujo wa tatu utakaofanyika Jumamosi, Agosti 29, katika Vipingo Ridge, Kaunti ya Kilifi.

Baada ya kufanyika kwa mafanikio katika duru mbili za awali mjini Limuru na Naivasha, msururu huo sasa unahamia Pwani ya Kenya, huku zaidi ya waendesha baiskeli 500 kutoka Kenya, Afrika Mashariki na mataifa mengine wakitarajiwa kushiriki. Washiriki watashindana katika mbio za kilomita 30, 55 na 105, huku usajili ukiendelea.

Waandalizi wameweka zawadi nono ambapo timu bingwa itajishindia Shilingi 125,000, nafasi ya pili Shilingi 100,000, na nafasi ya tatu Shilingi 70,000. Aidha, katika mbio za wasomi kwa wanaume na wanawake, washindi watano bora watatunukiwa zawadi za fedha kuanzia Shilingi 20,000 hadi Shilingi 5,000.

Mashindano hayo yanatarajiwa kuongeza hadhi ya Kenya kama kitovu cha michezo ya baiskeli barani Afrika na pia kuhamasisha utalii wa michezo kupitia mandhari ya kipekee ya Vipingo Ridge.

Muganda Jordan Schleck, aliyeshinda mashindano hayo Vipingo mwaka 2024 na 2025, atakuwa akiwania ubingwa wa tatu mfululizo. Hata hivyo, safari yake msimu huu imekuwa ngumu baada ya kushindwa kutwaa ushindi katika duru mbili zilizopita.

Akizungumza kuelekea mashindano hayo, Koordineta wa Mradi wa Amani, Troy Barrie, alisema mchujo wa Vipingo unaendelea kuonyesha dhamira ya waandalizi ya kuitangaza Kenya kama kitovu cha mashindano ya baiskeli duniani, huku ukiwapa waendesha baiskeli wa ndani fursa ya kushindana na wanariadha wa kiwango cha kimataifa.

Katika duru ya pili iliyofanyika Naivasha, Claudette Nyirarukundo wa Rwanda alishinda mbio za wanawake za kilomita 100 kwa muda wa saa 4:16:52, akimzidi Sarah Diekmeyer kwa sekunde moja pekee. Kwa upande wa wanaume, Lawrence Lorot wa Uganda mwenye umri wa miaka 21 aliibuka mshindi kwa muda wa saa 3:29:04, akimshinda Stanley Ngugi kwa tofauti ya sekunde moja katika fainali iliyokuwa ya ushindani mkubwa.


Share this to

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *