Share this to

By:Athuman Luchi

Wito wa kukomesha unyanyasaji dhidi ya wanawake umeendelea kutolewa, huku viongozi wakisisitiza umuhimu wa kulinda haki za wanawake na kuimarisha usawa wa kijinsia, ajenda ambayo imepewa kipaumbele katika mataifa mengi duniani.

Akizungumza jijini Mombasa, Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Mombasa, Zamzam Mohammed, alisema wanawake wengi bado wanakumbana na dhuluma zinazowanyima amani, usalama na fursa za maendeleo.

Amewahimiza wanawake wanaopitia vitendo vya unyanyasaji kutafuta msaada kupitia vyombo vya sheria na taasisi zinazotoa huduma za ulinzi na ushauri.

Kwa upande wake, Gavana wa Mombasa, Abdulswamad Nassir, amewataka wanaume kuachana na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na badala yake kushirikiana katika kujenga familia zenye heshima, usalama na maelewano.

Wakati huohuo, Zamzam amesema zaidi ya wasichana 350 waliokuwa wameacha masomo kutokana na mimba za utotoni wamefanikiwa kurejea shuleni kupitia juhudi za afisi yake, akieleza kuwa elimu ni nyenzo muhimu ya kuwawezesha wasichana na kupunguza changamoto zinazowakabili.

Kauli hizo zinajiri wakati juhudi za kimataifa zinaendelea kuhimiza kutokomezwa kwa ukatili wa kijinsia na kuimarishwa kwa fursa sawa za elimu na maendeleo kwa wanawake na wasichana duniani.


Share this to

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *