By:Alii Vincent

Wakazi wa eneo la Vikobani katika kaunti ndogo ya Jomvu, Mombasa, wanaendelea kunufaika na mpango wa Serikali ya Kaunti ya Mombasa wa kuwapatia hati miliki za ardhi, huku awamu ya pili ya utekelezaji wa mradi huo ikianza rasmi leo.
Mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Kaunti ya Mombasa na shirika la Geodev, ambapo awamu ya pili itahusisha ukusanyaji wa taarifa za wakazi na mali zao ili kuwezesha utoaji wa hati miliki kwa walionufaika pamoja na kuboresha upangaji wa matumizi ya ardhi katika eneo hilo.
Mshauri wa Geodev, Dennis Kimanthi, amesema zoezi hilo litatoa takwimu muhimu zitakazowasaidia wataalamu wa mipango miji kubaini huduma za msingi na miundombinu inayohitajika ili kuchochea maendeleo ya eneo la Vikobani.
Ameongeza kuwa lengo kuu la mpango huo ni kuhakikisha wakazi wanapata umiliki wa kisheria wa ardhi zao, hatua ambayo itaimarisha usalama wa umiliki wa ardhi na kutoa fursa za maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Kabla ya kuanza kwa awamu hiyo, Geodev iliandaa mkutano wa uhamasishaji katika Kanisa la Throne of Grace uliowakutanisha wakazi wote wa Vikobani, wakiwemo waliokwisha pimwa ardhi zao na wale ambao bado hawajapimwa, ili kuwapa maelezo kuhusu mchakato na umuhimu wa kushiriki katika zoezi hilo.
