By:Farida Ali

Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula, anakabiliwa na lawama nzito za kukiuka amri ya Mahakama Kuu inayomzuia kushiriki katika kampeni za kisiasa.
Kwenye kesi ya Kikatiba nambari E442 ya mwaka 2026 iliyowasilishwa na shirika la Vocal Africa, Jaji David Mburu alitoa amri ya muda mnamo tarehe 8 Julai, akimzuia Wetang’ula na Spika wa Seneti, Amason Kingi, kutumia ofisi zao kupigia debe chama chochote cha kisiasa ili kulinda uhuru wa Bunge.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Vocal Africa, Hussein Khalid, anasisitiza kuwa Wetang’ula alipokea amri hiyo rasmi kupitia barua pepe, mitandao ya kijamii, na ana kwa ana, lakini akaipuuza kwa makusudi.
Shirika hilo sasa linaitaka mahakama kumchukulia hatua kali Wetang’ula kwa dharau ya mahakama, wakisema kuwa kama wakili mkuu na kiongozi wa Bunge, anapaswa kuwa mstari wa mbele kuheshimu sheria.
Kesi hiyo inaendelea katika Idara ya Katiba na Haki za Kibinadamu Milimani.
