By:Hassan Pojo

Wakazi wa Wadi ya Ruruma, Rabai, Kaunti ya Kilifi, wamepata afueni baada ya kuzinduliwa kwa awamu ya saba ya ujenzi wa barabara ya kabro inayounganisha Mkapuni na Kadzuyuni.
Mbunge wa Rabai, Anthony Kenga Mupe, amesema mradi huo utaboresha usafiri, kurahisisha biashara na kusaidia wakulima kusafirisha mazao yao hadi sokoni.

Mupe amesema serikali ina mpango wa kuendeleza barabara hiyo kutoka Kadzuyuni hadi Masaani kwa kiwango cha lami, hatua itakayoongeza zaidi maendeleo katika eneo hilo.
Amewataka wakandarasi kuhakikisha kazi inakamilika kwa wakati na wananchi kulinda miradi ya maendeleo ili idumu.

Wakazi wamepongeza kuanza kwa mradi huo wakisema utapunguza changamoto za usafiri, hasa wakati wa mvua, na kuchochea shughuli za kiuchumi katika eneo hilo.
