Shirika la Reli la Kenya (KRC) limeeleza hatua kubwa zilizopigwa katika utekelezaji wa mradi wa treni mpya za kisasa zitakazohudumu jijini Mombasa, likilenga kuboresha usafiri wa umma na kupunguza msongamano barabarani.
Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati ya Bunge ya Utekelezaji katika Kituo cha Reli cha Mombasa na eneo la upakiaji katika Bandari ya Mombasa, Mkurugenzi Mkuu wa KRC, Bw. Philip Mainga, alisema kuwa treni hizo mpya ni sehemu ya mikakati mipana ya kuimarisha miundombinu ya usafiri wa reli mijini. Alibainisha kuwa treni hizo zitatoa huduma kati ya Stesheni ya Mombasa iliyokarabatiwa na Kituo Kikuu cha Miritini, kupitia vituo vya kati vya Changamwe Mashariki na Changamwe Magharibi.
“Mradi huu unalenga kuleta mapinduzi katika namna ambavyo watu wanatembea ndani ya jiji la Mombasa. Treni mpya za kisasa zitakuwa na uwezo wa kusafirisha abiria wengi kwa wakati mmoja, kwa bei nafuu na kwa muda mfupi ukilinganisha na magari ya binafsi au huduma za teksi,” alisema Bw. Maingi

Kwa mujibu wa Bw. Mainga ukarabati wa vituo vya reli pamoja na uwekaji wa miundombinu ya kisasa unakaribia kukamilika, huku Kituo cha Mombasa kikitarajiwa kufunguliwa rasmi ndani ya miezi miwili ijayo. Treni hizo mpya zitakuwa na mfumo wa kuhifadhi nafasi mapema, jambo litakalowarahisishia abiria kupanga safari zao kwa ufanisi.
Ingawa bei rasmi ya nauli haijatangazwa, Bw. Maingi alisisitiza kuwa gharama zitakuwa bei nafuu kwa wananchi ili kuhakikisha watu wengi wanamudu huduma hizo. “Lengo letu ni kutoa suluhisho la kudumu kwa changamoto ya usafiri, kwa kuweka viwango vya nauli vinavyowezekana kwa wananchi wa kawaida,” aliongeza.
Treni hizi mpya ni mwendelezo wa mafanikio yaliyoshuhudiwa kupitia huduma ya Madaraka Express, ambayo kwa mujibu wa Bw. Maingi, imesafirisha abiria karibu milioni mbili kwa mwaka ongezeko kubwa kutoka abiria 20,000 mwaka wa kwanza wa kuanzishwa kwake.
KRC inaendelea kushirikiana na serikali na wadau wengine katika kuhakikisha utekelezaji wa mradi huu unafanikishwa kwa wakati na kwa ubora unaohitajika.

