Share this to

By:Robert Mutasi

Seneta wa Nyandarua John Methu amemshutumu Mbunge wa Nakuru Town West Samuel Arama kwa madai ya kupanga vijana kuvuruga shughuli ya ufunguzi wa ofisi za chama cha Democracy for Citizens Party (DCP) mjini Nakuru.

Akizungumza na wanahabari mjini Nakuru Jumanne, Methu alisema amepokea taarifa za kiintelijensia kwamba Arama anaandaa kundi la vijana kusababisha vurugu wakati wa shughuli hiyo katika eneo bunge la Nakuru Town West.

Seneta huyo alikuwa ameandamana na viongozi wa DCP waliovalia mavazi ya kijani yenye picha ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, ambaye chama hicho kinahusishwa naye.

Methu ameitaka Polisi wa Kaunti ya Nakuru kuchukua hatua mapema, akisema taarifa hizo zinatolewa kwa lengo la kuzuia vurugu na kulinda maisha pamoja na mali ya wananchi.

“Tunataka kumjulisha Kamanda wa Kaunti ili usije ukadai kutokuwa na habari. Tunataka kukupa intelijensia. Samuel Arama anaandaa wahuni kuhujumu shughuli zetu za kufungua ofisi za chama chetu huko Nakuru Town West,” alisema Methu.

Methu alionya kuwa polisi hawapaswi kupuuza taarifa hizo, akisisitiza kuwa jukumu la kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao ni la vyombo vya usalama.

Seneta huyo pia alitoa madai mengine kuhusu mkutano wa DCP uliopangwa kufanyika Njoro, akidai kuwa Msaidizi wa Kibinafsi wa Mbunge wa Njoro, Shimiwa Kalambi, ameandaa vurugu kabla ya mkutano huo.

“Tumejulishwa kuwa msaidizi binafsi wa mbunge wa Njoro, Shimiwa Kalambi, pia ameandaa vurugu katika mkutano ambao tunatarajia kuhudhuria Njoro,” alisema.

DCP, chama kinachohusishwa na Gachagua, kimekuwa kikipanua shughuli zake nchini kwa kufungua ofisi katika maeneo mbalimbali kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

Viongozi wa chama hicho wamekuwa wakidai kukumbana na vitisho na upinzani katika baadhi ya maeneo wanakofanya shughuli za kisiasa.

Hata hivyo, hadi wakati wa kuchapisha habari hii, Samuel Arama alikuwa hajajibu madai hayo, huku Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Nakuru pia akiwa hajatoa taarifa rasmi kuhusu tuhuma hizo au mipango ya kiusalama kwa shughuli za DCP.


Share this to

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *