By:Hassan Pojjo

Mwanafunzi wa Gredi ya Tisa katika JCC Academy Likoni, Enock Musili, ameandika historia baada ya kutambuliwa kuwa mwamuzi (refa) mchanga zaidi katika Kaunti ya Mombasa, hatua inayodhihirisha ukuaji wa vipaji vya vijana katika sekta ya uamuzi wa soka.
Enock alikuwa miongoni mwa waamuzi waliopewa jukumu la kusimamia fainali za mashindano ya soka ya Junior Secondary School (JSS) ngazi ya Kaunti ya Mombasa, mechi iliyochezwa katika Uwanja wa Bomu Stadium mbele ya mamia ya mashabiki.
Utendaji wake umepongezwa na wadau wa michezo, viongozi wa elimu pamoja na waamuzi wenzake, waliomtaja kama mfano wa kuigwa kwa vijana wanaotamani kujenga taaluma katika uamuzi wa soka.

Wamesema mafanikio ya Enock yanathibitisha kuwa umri mdogo si kikwazo cha kufikia ndoto, mradi mtu awe na nidhamu, kujituma na kupata mafunzo pamoja na mwongozo unaofaa.
Uongozi wa JCC Academy Likoni umeeleza fahari yake kwa mafanikio hayo, ukisema utaendelea kuibua na kuendeleza vipaji vya wanafunzi katika michezo na shughuli nyingine za maendeleo ili kuwajengea mustakabali bora.
Kwa upande wao, wadau wa soka wamewataka wazazi, shule na vyama vya michezo kuwekeza zaidi katika kulea na kuwapa nafasi vijana wenye vipaji, wakisema hatua hiyo itasaidia kuongeza idadi ya waamuzi na viongozi wa michezo wenye weledi nchini.
Mafanikio ya Enock yameibua pongezi nyingi katika mitandao ya kijamii, ambapo wengi wamemtakia mafanikio zaidi na kueleza matumaini kuwa siku moja atakuwa miongoni mwa waamuzi bora wa soka nchini na hata katika mashindano ya kimataifa.
