Share this to

By:Hassan Pojjo

Mbunge wa Mvita, Mohammed Masoud Machele, ametangaza kukamilika kwa zoezi la ushirikishwaji wa umma kuhusu mpango wa maendeleo wa mwaka wa fedha 2026/2027, baada ya mkutano wa mwisho kufanyika katika eneo la Swahilipot, Wadi ya Old Town.

Akizungumza baada ya zoezi hilo, Machele alisema mikutano ilifanyika katika wadi zote tano za eneo bunge la Mvita, ambapo wakazi walipata fursa ya kutoa maoni na kuweka vipaumbele vyao kuhusu miradi ya maendeleo inayotarajiwa kutekelezwa katika mwaka wa fedha ujao.

Alisema ushiriki mkubwa wa wananchi unaonyesha dhamira yao ya kushiriki katika maamuzi yanayohusu maendeleo ya eneo lao. Aliongeza kuwa maoni yote yaliyokusanywa yatazingatiwa katika kuandaa mpango wa maendeleo unaolenga kukidhi mahitaji ya wakazi wa Mvita.

Mbunge huyo aliwashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi na kushiriki kikamilifu katika mikutano hiyo, akieleza kuwa mchango wao utasaidia kuhakikisha rasilimali za maendeleo zinaelekezwa kwenye miradi yenye manufaa kwa jamii.

Aidha, alisisitiza kuwa uongozi wake utaendelea kuzingatia misingi ya uwazi, uwajibikaji na ushirikishwaji wa wananchi katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo.

Machele alisema kupitia kaulimbiu ya “Huduma na Maendeleo,” ataendelea kushirikiana na wakazi wa Mvita kuimarisha sekta mbalimbali zikiwemo elimu, afya, miundombinu, uwezeshaji wa vijana na wanawake pamoja na huduma nyingine muhimu.

Pia aliwataka wakazi wa Mvita kuendelea kushirikiana na viongozi wao, akisema ushirikiano huo ndio msingi wa utekelezaji wa miradi yenye tija na inayokidhi matarajio ya wananchi.


Share this to

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *