Share this to

By:Robert Mutasi

Aliyekuwa Naibu wa Rais, Rigathi Gachagua, amewakemea aliyekuwa Mawaziri Justin Muturi na Peter Munya, akiwataka kuacha kulalamika kuwa chama chake cha Democracy for Citizens Party (DCP) kinatawala muungano wa upinzani na badala yake wajitahidi kuviuza vyama vyao kwa wananchi.

Akihutubia mkutano wa kisiasa Kaunti ya Meru siku ya Jumamosi, Gachagua alisema hakuna njia ya mkato ya kufaulu katika siasa na hakuna mbadala wa juhudi, akipuuza madai kuwa DCP inavifunika vyama vingine katika Muungano wa Upinzani wa Pamoja.

“Msiwe wavivu, viuzeni vyama vyenu vya kisiasa,” Gachagua alisema kwa msisitizo. “Sisi tuko na bidii. Hakuna njia ya mkato ya kazi ngumu. Hakuna mbadala wa juhudi.”

Gachagua, ambaye aliandamana na washirika wake wa kisiasa, alikuwa akijibu kauli zilizonasibishwa na Muturi, kiongozi wa chama cha Democratic Party (DP), na Munya, kiongozi wa Party of National Unity (PNU), ambao walidai kuwa DCP ya Gachagua inapewa nafasi kubwa kupita kiasi katika shughuli za upinzani eneo la Mlima Kenya.

Gachagua alifichua kuwa aliwahi kufanya mazungumzo ya faragha na Muturi ambapo walikubaliana jinsi ya kushirikiana, lakini akasema amesikitishwa na hatua ya aliyekuwa Mwanasheria Mkuu huyo kwenda hadharani kulalamika.

“Kweli nitazungumza na Muturi, tunasema mara moja, tuangalie tuvumiliane jinsi ya kufanya kazi pamoja,” Gachagua alisema, akisisitiza kuwa tofauti za ndani ya upinzani zinapaswa kutatuliwa kupitia majadiliano badala ya mashambulizi ya hadharani.

Aliyekuwa Naibu wa Rais alisisitiza kuwa umaarufu wa chama chake cha DCP unatokana na kuhamasisha wananchi mashinani na kujumuika nao moja kwa moja, na akawatahadharisha viongozi wenzake wa upinzani kuiga mfano huo badala ya kutegemea umaarufu wa DCP.

Alisema kuwa Wakenya sasa wamepevuka kisiasa na wataunga mkono vyama vyenye ajenda bayana na vilivyo na uwepo mashinani, na si vile vinavyoishia kwenye mikutano ya hoteli jijini Nairobi na taarifa kwa vyombo vya habari.

Kauli za Gachagua zinajiri wakati muungano wa upinzani unajitahidi kuimarisha uungwaji mkono wake katika eneo la Mlima Kenya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027. Muungano huo unaojumuisha viongozi kama Kalonzo Musyoka, Eugene Wamalwa na Fred Matiang’i umekuwa ukifanya mikutano ya pamoja nchini.

Hata hivyo, dalili za mvutano zimeanza kujitokeza kuhusu ushindani wa nani ataidhibiti ngome ya Mlima Kenya yenye kura nyingi. Muturi na Munya, wanasiasa wazoefu kutoka eneo hilo, wanaonekana kuwa washindani wa moja kwa moja wa Gachagua katika kuwania kura za Mlima Kenya Mashariki.

Wachambuzi wa siasa wanasema Gachagua ana nia ya kukifanya chama cha DCP kuwa chama chenye nguvu zaidi katika eneo hilo baada ya kutofautiana na Rais William Ruto na chama chake cha United Democratic Alliance (UDA). Kampeni zake za kuchapa kazi mashinani zimemvutia umati mkubwa, hatua ambayo imewatikisa wanasiasa wengine wa eneo hilo.

Gachagua alisisitiza kuwa kuna nafasi tosha kwa vyama vyote kuishi pamoja na kukua, lakini ni lazima viongozi wajitume.

“Kila mtu lazima afanye kazi kwa bidii. Nendeni kwa wananchi, elezeni sera zenu. Huwezi kukaa Nairobi na kutarajia wananchi wakufuate,” aliongeza.

Hadi wakati wa kuandikwa kwa taarifa hii, Muturi na Munya hawakuwa wamejibu kauli hizo za Gachagua.


Share this to

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *