By:Gloria Mwaganda

Shirika la Kenya Community Support Centre (KECOSCE) kwa ushirikiano na mashirika mbalimbali ya kiraia limezindua rasmi mradi wa IMARISHA, unaolenga kuimarisha uongozi wa wanawake na kuongeza ushiriki wao katika masuala ya amani, usalama na maendeleo ya jamii katika ukanda wa Pwani.
Mradi huo utatekelezwa katika kaunti za Kilifi, Mombasa na Kwale, ukiwa na dhamira ya kuwajengea wanawake uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maamuzi yanayohusu jamii, kuimarisha juhudi za kuzuia migogoro na kukuza maendeleo jumuishi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo mjini Kilifi, Afisa wa Mradi wa KECOSCE, Fauzia Kasim, alisema IMARISHA inalenga kuhakikisha wanawake wanapata nafasi sawa ya kushiriki katika uongozi na michakato ya maamuzi kuanzia ngazi ya mashinani hadi ya juu.
Alisema tathmini zilizofanywa katika ukanda wa Pwani zimeonyesha kuwa wanawake wengi bado wanakabiliwa na changamoto za kijamii, kiuchumi na kiutamaduni zinazowazuia kushiriki kikamilifu katika masuala ya uongozi, amani na usalama.
Kwa mujibu wa Kasim, mradi huo utawajengea wanawake uwezo wa uongozi, kuwapa mafunzo ya utatuzi wa migogoro, kuwawezesha kushiriki katika juhudi za kudumisha amani na kuimarisha uwezo wao wa kujitegemea kiuchumi.
“Jamii yenye amani na maendeleo endelevu haiwezi kujengwa bila ushiriki wa wanawake katika kufanya maamuzi. Mradi huu unalenga kuhakikisha wanawake wanakuwa sehemu ya suluhisho la changamoto zinazoikabili jamii,” alisema.
Aliongeza kuwa utekelezaji wa mradi utahusisha ushirikiano wa karibu na machifu, viongozi wa kijamii, mashirika yanayoongozwa na wanawake pamoja na wadau wengine ili kuhakikisha manufaa ya mradi yanawafikia wananchi katika ngazi ya vijiji. Aidha, alisema wanaume na vijana wa kiume pia watahusishwa kikamilifu kwa kuwa usawa wa kijinsia na amani vinahitaji ushirikiano wa jamii nzima.
Kwa upande wake, Waziri wa Kaunti anayeshughulikia masuala ya Jinsia, Ruth Dama, alisema mradi huo unaunga mkono juhudi za serikali ya kaunti za kulinda haki za wanawake na kupambana na ukatili wa kijinsia.
Alifichua kuwa Kaunti ya Kilifi imerekodi visa 939 vya ukatili wa kijinsia, huku baadhi ya waathiriwa wakiendelea kukosa huduma na haki wanazostahili. Alisema hali hiyo inaonyesha umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya serikali, mashirika ya kiraia na jamii katika kuzuia na kushughulikia visa hivyo.
Dama alisema serikali ya kaunti inalenga kuwawezesha wanawake kushiriki zaidi katika mifumo ya usalama wa jamii na michakato ya maamuzi ili kujenga jamii salama na yenye usawa.
Aidha, alibainisha kuwa juhudi za pamoja kati ya serikali, wazazi na viongozi wa jamii zimechangia kupungua kwa baadhi ya vitendo vya ukatili dhidi ya watoto. Hata hivyo, aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana katika kutokomeza ukatili wa kijinsia, mawozo, kupotea kwa watoto na vitendo vingine vinavyohatarisha usalama wa watoto na vijana.
Kadri Kenya inavyoelekea katika kipindi cha uchaguzi mkuu ujao, Dama alisisitiza umuhimu wa kuwaelimisha vijana kuhusu mshikamano wa kitaifa, uvumilivu wa kisiasa na njia za amani za kushiriki katika mchakato wa kidemokrasia ili kuzuia migogoro na vurugu zinazoweza kujitokeza.
Mradi wa IMARISHA unatarajiwa kuimarisha mifumo ya amani katika jamii za ukanda wa Pwani kwa kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi, maamuzi na juhudi za kujenga jamii salama, jumuishi na yenye maendeleo endelevu.
