Share this to

By:Farida Ali

Gavana wa Mombasa, Abdullswamad Sheriff Nassir, amekanusha madai ya Waziri wa Afya, Aden Duale, kwamba hospitali za umma katika kaunti hiyo zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa dawa.

Akizungumza katika Hospitali ya Rufaa ya Coast General, Nassir amesema takwimu zilizowasilishwa na Waziri Duale zilijumuisha vituo vyote 239 vya afya vilivyopo Mombasa, vikiwemo vya kibinafsi, na hivyo hazikupaswa kutumiwa kutathmini hali ya hospitali za umma pekee.

Amesema Serikali ya Kaunti ya Mombasa inasimamia vituo 52 vya afya, akibainisha kuwa upatikanaji wa dawa katika vituo hivyo umefikia asilimia 92.

Kwa mujibu wa gavana huyo, asilimia iliyobaki ya dawa ambazo hazipatikani kwa wakati hutokana na changamoto za usambazaji kutoka kwa wasambazaji au ucheleweshaji wa utoaji wa baadhi ya bidhaa maalumu za matibabu, huku akisisitiza kuwa kaunti inaendelea kushughulikia hali hiyo ili kuhakikisha huduma hazitatizwi.

Nassir ameeleza kuwa serikali ya kaunti imeendelea kuwekeza katika ununuzi wa dawa na vifaa tiba pamoja na kuimarisha mfumo wa usambazaji ili kuhakikisha wagonjwa wanaopokea huduma katika hospitali za umma hawakosi dawa muhimu.

Aidha, amewataka wakosoaji na wadau wa sekta ya afya kutenganisha takwimu za vituo vya umma na vile vya kibinafsi ili kutoa tathmini sahihi ya utendakazi wa huduma za afya katika kaunti hiyo.

Amesisitiza kuwa tathmini za sekta ya afya zinapaswa kuzingatia takwimu sahihi ili kuepusha kutoa taswira isiyoakisi hali halisi ya huduma zinazotolewa kwa wananchi.


Share this to

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *