By:Alii Vincent

Kenya inatarajia kuweka historia duniani Jumapili kwa kujaribu kuvunja rekodi ya Guinness World Records kupitia zoezi la kupanda miche 5,000 ya mikoko ndani ya saa moja.
Jaribio hilo linaandaliwa na Chama cha Skauti nchini (Kenya Scouts Association) kwa ushirikiano na M-Pesa Foundation, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Miti ya Mikoko.
Mamii ya vijana wa Skauti wanatarajiwa kushiriki katika zoezi hilo litakalofanyika Jomvu Kuu, Kijiji cha Kwa Fara, Kaunti ya Mombasa, kuanzia saa moja na nusu asubuhi.

Waandalizi wanasema lengo ni kupanda miche 5,000 ya mikoko ndani ya saa moja, hatua inayokusudiwa kuimarisha uhifadhi wa mazingira ya bahari, kulinda mifumo ya ikolojia ya pwani na kuunga mkono juhudi za kimataifa za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Endapo jaribio hilo litafanikiwa, Kenya itaandika historia kwa kujiunga na mataifa yaliyoweka rekodi za kimataifa kupitia shughuli za uhifadhi wa mazingira, huku ikiangazia umuhimu wa mikoko katika kukabiliana na ongezeko la joto duniani na kuhifadhi bioanuwai ya bahari.
