By:Glory Mwagambo

Wakazi wa Malindi katika Kaunti ya Kilifi wamelalamikia hali mbaya ya Barabara ya Tsavo, wakisema imegeuka kuwa chanzo cha ajali za mara kwa mara na kero kubwa kwa watumiaji wa barabara hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya wakazi, Philip Baraka, ambaye anaishi karibu na Barabara ya Tsavo, amesema kuwa barabara hiyo imeharibika kutokana na mashimo makubwa yaliyosambaa katika sehemu mbalimbali. Amesema hali hiyo imekuwa changamoto kwa wakazi, wafanyabiashara na watalii wanaotembelea mji wa Malindi.
Baraka ameeleza kuwa ubovu wa barabara umeathiri shughuli za kiuchumi, huku gharama za usafirishaji wa bidhaa zikiongezeka kutokana na ugumu wa kupita katika eneo hilo. Pia amewataka madereva na watumiaji wengine wa barabara kuwa waangalifu ili kupunguza ajali zinazoendelea kushuhudiwa.
Kauli hiyo imeungwa mkono na Moris Omondi, ambaye amesema wakazi wamekuwa wakiiomba serikali na mamlaka husika kukarabati barabara hiyo kwa muda mrefu bila mafanikio.
Kwa mujibu wa Omondi, hali ya barabara imekuwa kikwazo kikubwa katika kuwahudumia wagonjwa, kwani mara nyingi magari ya kubeba wagonjwa hupata ugumu wa kupita, jambo ambalo linaweza kuhatarisha maisha ya wagonjwa wanaohitaji huduma za dharura.
Aidha, wakazi hao wamesema kuwa wakati wa mvua, mashimo hujaa maji na hivyo kufanya iwe vigumu kwa madereva kutambua maeneo hatari, hali inayoongeza hatari ya kutokea kwa ajali.
Wakazi hao sasa wameiomba serikali pamoja na idara zinazohusika na miundombinu kuchukua hatua za haraka za kukarabati Barabara ya Tsavo ili kurejesha usalama wa watumiaji wa barabara hiyo na kuchochea shughuli za kiuchumi katika mji wa Malindi.
