By:Hassan Pojjo

Timu ya Kalalani Combined kutoka Mwavumbo, Mariakani, Kaunti ya Kwale, inaendelea kujijengea jina kama jukwaa la kukuza vipaji vya soka kwa vijana kupitia mechi za kirafiki na mashindano ya mitaani.
Mwanzilishi wa timu hiyo, Timna Dzame, amesema aliianzisha baada ya kuona vijana wengi wenye vipaji wakikosa nafasi ya kushiriki katika ligi rasmi za Shirikisho la Soka Kenya (FKF). Kupitia Kalalani Combined, amesema vijana hao wanapata fursa ya kuonyesha uwezo wao na kuonekana na makocha pamoja na wadau wa soka.
Dzame alieleza kuwa mbali na kukuza vipaji, timu hiyo inalenga kuimarisha umoja, nidhamu na mshikamano miongoni mwa vijana kwa kutumia michezo kama chombo cha maendeleo ya kijamii.
Benchi la ufundi linaongozwa na Kim Mwachia na Kombo Chitibwa, huku wachezaji wa zamani wa eneo hilo wakijitolea kuwanoa na kuwashauri vijana.
Mazoezi hufanyika katika Uwanja wa Kalalani, ambapo wachezaji hujifua kiufundi na kujiandaa kwa mechi mbalimbali. Juhudi hizo zimeanza kuzaa matunda, huku timu ikirekodi matokeo mazuri, ikiwemo ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Young Tigers FC katika mchezo wa kirafiki.
Viongozi wa Kalalani Combined sasa wanatoa wito kwa wadau wa michezo kuunga mkono juhudi zao ili kuwasaidia vijana wengi zaidi kutimiza ndoto za kucheza katika ligi za juu nchini na kimataifa.
