Share this to

By:Betty Luke

Shirikisho la Riadhia la Kenya, Athletics Kenya, limezindua rasmi mfumo mpya wa kisasa ujulikanao kama Athlete Hub, ambao unalenga kubadilisha kabisa usimamizi wa riadha, kuimarisha maadili na kurejesha heshima ya Kenya katika riadha za kimataifa.

Mfumo huo wa mageuzi umezinduliwa katika hafla ya kihistoria iliyofanyika Eldoret, iliyoongozwa na Rais wa Athletics Kenya, Jenerali Mstaafu Jackson Tuwei, ambaye pia ni Makamu wa Rais wa World Athletics, pamoja na maafisa kutoka Wizara ya Michezo, Kitengo cha Maadili cha World Athletics (AIU), makocha na wanariadha wa zamani na waliopo.

Katika hotuba yake, Jenerali Tuwei alikumbusha historia ya matumizi ya dawa za kusisimua misuli nchini, akisema kisa cha kwanza kilirekodiwa miaka 40 iliyopita na ndicho kilichotufikisha tulipo leo katika Kundi A, chini ya sheria za kupambana na matumizi ya dawa hizo.

“Na uhakika nyote mnakumbuka kisa cha kwanza cha matumizi ya dawa za kusisimua nchini Kenya miaka 40 iliyopita. Ndipo historia ya doping ilipoanzia. Na sasa tuko Kundi A kwa sababu ya changamoto hizi,” alisema Tuwei.

Alisema kuzinduliwa kwa Athlete Hub ni hatua ya makusudi ya kuandika historia mpya ya kutoka kwenye Kundi A na kurejesha imani ya dunia kwa wanariadha wa Kenya.

Mfumo huo wa kidijitali utakusanya huduma zote muhimu katika sehemu moja salama. Hizi ni pamoja na usajili wa wanariadha, usimamizi wa makocha na wasaidizi wengine, usimamizi wa mashindano, ufuatiliaji wa vipaji, usimamizi wa kambi za mazoezi, na huduma za visa kwa wanariadha wanaokwenda mashindano ya nje.

Kwa mujibu wa Tuwei, mfumo huo utarahisisha upatikanaji wa huduma kwa wanariadha bila urasimu mwingi wa makaratasi, huku ukihakikisha makocha, mameneja, madaktari na wataalamu wengine wanaohudumia wanariadha wamesajiliwa na kuthibitishwa kisheria.

Bingwa wa Olimpiki mara mbili, Eliud Kipchoge, alitoa wito mzito kwa wanariadha kuzingatia uaminifu. Alisema Kenya sasa inapaswa kushinda medali ya aina nyingine — medali ya imani.

“Kuna mbio mbili muhimu. Ya kwanza ni mbio ambayo kila mtu anaiona, ya kushindana na wengine na saa. Ya pili ni mbio ya imani. Mbio hii huanza muda mrefu kabla ya bunduki ya kuanza kulia na huendelea hata baada ya kumaliza mbio,” alisema Kipchoge.

Alibainisha kuwa kufikia mwanzoni mwa 2025, Wakenya walikuwa 140 kati ya majina 680 kwenye orodha ya AIU duniani — takriban mmoja kati ya kila watano — hali inayofanya kila ushindi wa Mkenya kutazamwa kwa mashaka.

Kipchoge aliwataka wanariadha kuchukua jukumu binafsi, kuwa makini na nani wanaomuamini na kutobeba kimya uovu.

“Mwili wako ni kazi yako. Kipaji kinaweza kukufikisha jukwaani, lakini uwajibikaji ndio utakao kuweka hapo na jina lako likiwa safi,” aliongeza.

Aliwataka makocha, madaktari, wataalamu wa viungo na mawakala kumlinda mwanariadha kwanza kabla ya kutafuta matokeo.

Kituo hicho kimejengwa Eldoret, kitovu cha riadha duniani, na kinatarajiwa kuleta elimu, upimaji, taarifa na msaada karibu na wanariadha, na hivyo kulinda mustakabali wa riadha ya Kenya.


Share this to

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *