Share this to

By:Farida Ali

Mamlaka ya Mawasiliano nchini, CA, imefafanua masharti mapya ya leseni kwa vituo vya huduma za intaneti vya umma, maarufu kama Cyber Café.

CA imesema masharti hayo yanalenga kuimarisha usalama na uwajibikaji katika matumizi ya intaneti, bila kuathiri haki ya wananchi kupata huduma za kidijitali.

Kanuni hizo zilichapishwa katika Gazeti la Serikali tarehe 7 Agosti 2026 na zinatarajiwa kuanza kutumika rasmi Septemba 7, 2026.

Chini ya masharti hayo, wamiliki wa Cyber Café watatakiwa kuthibitisha utambulisho wa wateja, kuweka wazi bei za huduma na kutoa risiti kwa huduma zote zinazolipiwa.

Aidha, vituo hivyo vitatakiwa kuhifadhi taarifa za msingi za matumizi ya kompyuta, ikiwemo namba ya kompyuta iliyotumiwa pamoja na muda ambao mteja alianza na kumaliza kutumia huduma.

Hata hivyo, CA imesisitiza kuwa wamiliki wa Cyber Café hawatalazimika kuhifadhi historia ya tovuti ambazo wateja wanatembelea wala jumbe zao binafsi.

Mamlaka hiyo pia imefafanua kuwa sheria hizo hazilazimishi matumizi ya mfumo maalum wa utambulisho wala uwekaji wa kamera za CCTV.

CA imesema hatua hizo ni sehemu ya juhudi za kukabiliana na uhalifu wa mtandaoni, ikiwemo utapeli, wizi wa utambulisho na udanganyifu unaoweza kufanywa kupitia kompyuta za umma.

Mamlaka hiyo imewataka wamiliki wa Cyber Café kufahamu masharti hayo mapya, huku ikiahidi kushirikiana nao kuhakikisha utekelezaji wa kanuni hizo hauathiri biashara wala upatikanaji wa huduma za kidijitali kwa wananchi.


Share this to

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *