Share this to

By:Hassan Pojjo

Al Shifaa Football Club imetwaa ubingwa wa Dola Super Cup kwa mara ya pili, ikiendeleza utawala wake katika mashindano hayo na kujiimarisha miongoni mwa timu zinazofanya vizuri katika soka la jamii na Kaunti ya Mombasa.

Ushindi huo umefika katika kilele cha makala ya pili ya Dola Super Cup, mashindano yaliyoshirikisha jumla ya timu 24 katika kipindi cha takribani mwezi mmoja.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Soka Kaunti ya Mombasa, Alamin Ahmed Abdallah, amewapongeza wachezaji wa Al Shifaa, benchi la ufundi pamoja na mashabiki wa timu hiyo kwa mafanikio hayo.

Alamin amesema mafanikio ya Al Shifaa yanaonyesha umuhimu wa mashindano ya ndani katika kuwapa wachezaji nafasi ya kuonyesha vipaji vyao, kupata uzoefu na kujenga msingi wa safari zao za kisoka.

Amepongeza Dola Group of Companies kwa udhamini wa mashindano hayo, akisema Dola Super Cup imekuwa jukwaa muhimu la burudani, ushindani na ukuzaji wa vipaji vya soka katika ukanda wa Pwani.

Kwa mujibu wa Alamin, ushirikiano kati ya sekta binafsi, taasisi za michezo na serikali unaweza kuchangia pakubwa katika kujenga mazingira bora ya maendeleo ya soka na kuwafungulia vijana fursa zaidi.

Amesema mashindano hayo yamewapa wachezaji kutoka viwango na madaraja tofauti fursa ya kuonyesha uwezo wao mbele ya mashabiki, makocha na wadau wa soka.

Alamin pia ametoa pongezi kwa Football Kenya Federation (FKF) na Mombasa Sports Club kwa mchango wao katika uratibu na kufanikisha mashindano hayo.

Amesema mashindano kama Dola Super Cup yanapaswa kupewa nafasi zaidi kwa kuwa, mbali na kutoa burudani, yanasaidia pia kugundua na kukuza vipaji vya vijana.

KAUNTI YAPONGEZA UWEKEZAJI KATIKA VIJANA

Kwa upande wake, CECM wa Vijana, Jinsia na Michezo, Jonathan Kutosi Wepukhulu, amepongeza Dola Group of Companies kwa kuendelea kuwekeza katika programu zinazowahusisha vijana kupitia michezo.

Wepukhulu amesema michezo ni nyenzo muhimu ya kuwaunganisha vijana, kukuza vipaji na kuwaweka katika shughuli chanya zinazoweza kuwajengea maisha bora ya baadaye.

Serikali ya Kaunti ya Mombasa imesema uwekezaji katika michezo pia unaweza kusaidia kukabiliana na changamoto zinazowakabili vijana, ikiwemo kujiunga na makundi ya kihalifu na kushiriki katika vitendo vinavyoweza kuhatarisha mustakabali wao.

Wadau wa soka wameitaka Dola Group of Companies kuendelea na uwekezaji huo, wakisema Dola Super Cup ni mfano wa namna sekta binafsi inavyoweza kutumia michezo kama chombo cha maendeleo ya jamii.

Baada ya mafanikio ya makala ya pili, matarajio ya wadau ni kuona mashindano hayo yakipanuka zaidi na kuwafikia vijana wengi zaidi katika maeneo mbalimbali ya Mombasa na ukanda wa Pwani.


Share this to

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *