By:Hassan Pojjo

Watumiaji wa Barabara ya Kinango–Kwale wametakiwa kuwa waangalifu kufuatia kuharibika kwa sehemu ya Daraja la Marere (Manolo), hali ambayo imeibua wasiwasi kuhusu usalama wa wasafiri wanaotumia barabara hiyo.
Kwa mujibu wa wakazi wa eneo hilo, sehemu ya katikati ya daraja imeharibika, na kufanya matumizi ya barabara hiyo kuwa hatari, hasa kwa magari makubwa, waendesha pikipiki na wasafiri wanaosafiri nyakati za usiku au wakati wa mvua.
Kutokana na hali hiyo, mamlaka husika zimeanza kuandaa njia mbadala (diversion) ili kuwezesha magari na watumiaji wengine kuendelea na safari zao huku wakisubiri matengenezo ya kudumu ya daraja hilo.
Wananchi wamewataka madereva kupunguza mwendo wanapokaribia eneo hilo, kufuata alama za usalama na maelekezo ya maafisa wa trafiki pamoja na kutumia njia mbadala kwa tahadhari ili kuepusha ajali.
Wakazi pia wamezitaka mamlaka zinazohusika na miundombinu kuharakisha ukarabati wa Daraja la Marere, wakieleza kuwa Barabara ya Kinango–Kwale ni kiungo muhimu cha usafirishaji wa abiria, bidhaa na huduma muhimu katika Kaunti ya Kwale.
Kwa sasa, watumiaji wote wa barabara hiyo wanashauriwa kuwa waangalifu wanapopita katika eneo la Marere (Manolo) na kuzingatia maelekezo yaliyowekwa hadi matengenezo yatakapokamilika na usalama kurejea kikamilifu.
