By:Hassan Pojjo

Muwania wa kiti cha Ubunge wa Msambweni kwa tiketi ya Jubilee Party, Omar Mwalago, amesema atatanguliza maslahi ya wananchi kupitia uongozi wa uwazi, uwajibikaji na ushirikishwaji wa jamii iwapo atachaguliwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.
Akizungumza katika eneo bunge la Msambweni, Mwalago alisema atashirikiana kwa karibu na wananchi kubaini na kutatua changamoto zinazolikabili eneo hilo, akisisitiza kuwa maendeleo ya kweli yanahitaji ushirikiano kati ya viongozi na wananchi pamoja na matumizi ya uwazi wa rasilimali za umma.
Alibainisha kuwa vipaumbele vyake vikuu ni kuboresha sekta za elimu, afya na miundombinu, kuongeza fursa za ajira kwa vijana, kuwawezesha wanawake kiuchumi na kuimarisha mazingira ya biashara kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati.
Mwalago alisema Msambweni ina rasilimali na fursa nyingi za kiuchumi ambazo zinaweza kubadilisha maisha ya wananchi endapo zitasimamiwa kwa uongozi wenye maono na mipango madhubuti ya maendeleo.
Aidha, aliahidi kuendelea kufanya mashauriano na wakazi wa maeneo mbalimbali ya Msambweni ili kuhakikisha sauti na mahitaji yao yanazingatiwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Pia aliwataka wananchi kudumisha amani, mshikamano na umoja huku wakishiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo, akieleza kuwa ushirikiano kati ya viongozi na wananchi ndio msingi wa kuharakisha maendeleo ya eneo hilo.
Kauli hiyo inajiri huku shughuli za kisiasa zikizidi kushika kasi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027, ambapo viongozi mbalimbali wanaendelea kujinadi na kuwasilisha sera zao kwa wananchi katika sehemu tofauti za nchi.
