
By:Alii Vincent
Wakazi wa Kaliang’ombe katika eneo bunge la Rabai, Kaunti ya Kilifi, wameitaka serikali kuharakisha mchakato wa fidia kwa wananchi wanaodai kuathiriwa na milipuko ya baruti inayotumiwa na kampuni ya Victoria Mining.
Wakizungumza katika mkutano ulioongozwa na Naibu Kamishna wa Kaunti Ndogo (DCC) wa Rabai, Nicholus Kijuba, wakazi hao walisema kuwa tangu mwezi Februari kampuni hiyo imekuwa ikiahidi kulipa fidia bila hatua yoyote ya utekelezaji.
Wakazi hao wameitaka serikali kuharakisha uchapishaji katika Gazeti Rasmi la Serikali wa kamati iliyochaguliwa na wananchi, ili kuwezesha mchakato wa fidia kuanza kwa kiwango kilichokubaliwa kati ya pande husika. Mwenyekiti wa kamati hiyo, Ambrose Kalongo, alisema wananchi wamechoshwa na kucheleweshwa kwa mchakato huo.
Baadhi ya wajumbe wa kamati pia walielezea masikitiko yao wakisema kampuni hiyo imekuwa ikilichukulia suala hilo kwa uzito mdogo licha ya athari zinazoendelea kuwakumba wakazi.
Mbali na fidia, wananchi wameitaka serikali kuhakikisha kampuni hiyo inatenga fedha za ukarabati wa nyumba zao kila mwaka kutokana na nyufa zinazosababishwa na milipuko ya baruti.
Akizungumza katika mkutano huo, DCC Nicholus Kijuba aliwahakikishia wakazi kuwa ofisi yake itafuatilia kwa karibu hatua zote zilizobaki ili kuhakikisha wananchi wanapata haki yao. Pia aliwahimiza kuendelea kushirikiana na kampuni hiyo ili shughuli za uchimbaji ziweze kuendelea na hivyo kuwawezesha wananchi kunufaika na asilimia moja ya mapato ya kampuni kupitia miradi ya maendeleo ya jamii.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Victoria Mining alisema kampuni hiyo iko tayari kushirikiana na ofisi ya DCC ili kukamilisha hatua zilizobaki na kuhakikisha suala la fidia linapatiwa ufumbuzi.
