Share this to

By:Hassan Pojjo

Wakazi wa Wadi ya Miritini, katika Eneo Bunge la Jomvu, wamejitokeza kwa wingi kushiriki kikao cha ushirikishwaji wa umma kilicholenga kukusanya maoni kuhusu miradi ya maendeleo itakayofadhiliwa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Maeneo Bunge (NG-CDF) kwa kipindi cha miaka ya fedha 2026 hadi 2028.

Kikao hicho kilifanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi ya Miritini Comprehensive na kuhudhuriwa na Mbunge wa Jomvu, Badi Twalib, pamoja na mwakilishi wa Wadi ya Miritini, Kibwana Swaleh Baya, na viongozi wengine wa eneo hilo.

Akizungumza katika mkutano huo, Mbunge Badi Twalib aliwashukuru wananchi kwa kujitokeza na kutumia nafasi hiyo kueleza changamoto, mapendekezo na vipaumbele vyao kuhusu miradi wanayopendekeza kutekelezwa katika kipindi kijacho.

Alisema ushiriki wa wananchi ni muhimu katika kuhakikisha fedha za NG-CDF zinaelekezwa kwenye miradi yenye manufaa ya moja kwa moja kwa jamii, huku maamuzi yakizingatia mahitaji halisi ya wakazi.

Twalib alieleza kuwa mapendekezo yaliyotolewa yatafanyiwa tathmini na kuzingatiwa wakati wa kupanga bajeti na utekelezaji wa miradi, akisisitiza kuwa lengo ni kuhakikisha kila fedha inayotengwa inaleta mabadiliko chanya kwa wananchi.

Kwa upande wake, MCA wa Miritini, Kibwana Swaleh Baya, aliwahimiza wakazi kuendelea kushiriki katika mikutano ya maendeleo, akisema maoni yao yanasaidia viongozi kubuni miradi yenye tija na kuongeza uwazi katika matumizi ya rasilimali za umma.

Katika kikao hicho, wananchi walipendekeza miradi mbalimbali ikiwemo uboreshaji wa barabara, ujenzi na ongezeko la madarasa katika shule, kuimarisha huduma za afya, uwezeshaji wa vijana na wanawake kupitia miradi ya kiuchumi, pamoja na kuimarisha usalama na huduma za kijamii.

Viongozi hao waliwahakikishia wananchi kuwa maoni yote yaliyotolewa yamepokelewa na kurekodiwa, huku wakiahidi kuendelea kushirikiana na jamii kuhakikisha miradi itakayochaguliwa inatekelezwa kwa uwazi, ufanisi na kulingana na mahitaji ya wakazi.

Kikao hicho ni sehemu ya mfululizo wa mikutano ya ushirikishwaji wa umma inayoendelea katika wadi zote za Jomvu, ikiwa na lengo la kuwapa wananchi nafasi ya kushiriki moja kwa moja katika kupanga vipaumbele vya maendeleo kupitia fedha za NG-CDF kwa miaka ya fedha 2026–2028.


Share this to

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *