By:Hassan Pojo

Shirika la kijamii la Uhaki naa Usawa, kupitia Mkurugenzi wake Salim Suleiman, limeelezea wasiwasi mkubwa kuhusu kuongezeka kwa mrundikano wa taka katika jaa la taka la Chaani, eneo la Changamwe, Kaunti ya Mombasa, akisema hali hiyo imekuwa tishio kubwa kwa afya ya wakazi na mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.

Kwa mujibu wa Salim Suleiman, jaaa hilo lipo karibu sana na makazi ya wananchi, kituo cha Elimu ya Awali (ECDE) pamoja na shule ya sekondari, jambo ambalo limewafanya wanafunzi na walimu kulazimika kusomea katika mazingira yenye harufu kali, moshi na uvamizi wa nzi kila siku.

Amesema hali hiyo imeathiri kwa kiasi kikubwa ubora wa elimu kutokana na usumbufu unaosababishwa na taka hizo, huku ikihatarisha afya ya wanafunzi, walimu na wakazi wa maeneo yanayolizunguka dampo hilo.
Aidha, Salim amesema kumekuwa na ongezeko la magonjwa yanayohusishwa na uchafu na taka katika jamii, huku watoto, walimu na familia zinazoishi karibu na eneo hilo zikiwa waathirika wakubwa wa tatizo hilo la kimazingira.
Amesisitiza kuwa mazingira safi na salama si anasa bali ni haki ya msingi kwa kila mwananchi, na kwamba serikali ina wajibu wa kuhakikisha wananchi wanaishi katika mazingira yanayolinda afya na ustawi wao.

Kutokana na hali hiyo, Shirika la Uhaki na Usawa limetoa wito kwa Serikali ya Kaunti ya Mombasa kuchukua hatua za haraka kwa kuondoa taka zote zilizokusanyika katika dampo la Chaani bila kuchelewa.
Shirika hilo pia limetaka kuwepo kwa mpango wa kudumu na endelevu wa usimamizi wa taka ili kuzuia tatizo hilo kujirudia na kuhakikisha afya pamoja na elimu ya wananchi wa Changamwe inalindwa.
Kwa mujibu wa shirika hilo, wakazi wa Changamwe wanastahili huduma bora za usafi pamoja na mazingira salama yanayofaa kwa makazi ya binadamu na maendeleo ya kijamii.

Kauli hiyo imeungwa mkono na mashirika mbalimbali ya kijamii na watetezi wa haki za binadamu, yakiwemo VOCAL Africa, HAKI Africa, Social Justice Centers Working Group, Mukuru Community Justice Center, Amkeni Community Organisation, Sisters for Justice, IJM Kenya pamoja na wadau wengine wanaoshirikiana katika masuala ya haki za kijamii, mazingira na utawala bora.
Mashirika hayo yamehimiza mamlaka husika kuchukua hatua za haraka ili kulinda afya, elimu na ustawi wa wakazi wa Changamwe.
.
