By:Glory Mwangambo

Hali ya uchafu unaotokana na maji taka yanayotuama kwenye mitaro katika eneo la Stage Mpya mjini Malindi, Kaunti ya Kilifi, imezua wasiwasi miongoni mwa washikadau wa sekta ya usafiri na wafanyabiashara, ambao wanasema tatizo hilo linahatarisha afya zao na za wananchi.
Wakizungumza na Kilele Radio, walisema mitaro hiyo imejaa maji taka kwa muda mrefu, hali inayosababisha harufu mbaya, kuzaliana kwa mbu na kuongeza hofu ya kuenea kwa magonjwa.
Mmoja wa wafanyabiashara katika eneo hilo, Lazarus Chome, amesema licha ya kuwasilisha malalamiko yao mara kadhaa kwa mamlaka husika, hakuna hatua madhubuti iliyochukuliwa kutatua tatizo hilo. Aidha, amedai kuwa Idara ya Manispaa haijafanya usafi wa mitaro hiyo kwa muda mrefu.
Chome ameongeza kuwa tatizo hilo si la Stage Mpya pekee, bali pia linaonekana katika maeneo mengine ya mji wa Malindi ambayo, kwa mujibu wake, yamepuuzwa na kukosa huduma za usafi kwa muda mrefu.
Amesema wafanyabiashara hulazimika kutumia dawa za kuzuia wadudu kila siku kabla ya kuanza shughuli zao ili kujikinga dhidi ya magonjwa, huku mazingira machafu na harufu kali vikifanya iwe vigumu kufanya biashara.
Washikadau hao sasa wameiomba Serikali ya Kaunti ya Kilifi pamoja na mamlaka husika kuchukua hatua za haraka kusafisha mitaro hiyo na kuweka mfumo endelevu wa usimamizi wa taka na maji taka ili kulinda afya ya wananchi na kuboresha mazingira ya biashara.
