
Mashindano ya soka yanayodhaminiwa na Elkana Jacob, yanayolenga kuibua vipaji vya vijana, kuhamasisha amani na kuimarisha mshikamano katika eneo la Nyali, yanatarajiwa kuanza rasmi hivi karibuni.
Mashindano hayo yatakayoshirikisha timu kutoka kata zote tano za eneo bunge la Nyali, ambazo ni Kongowea, Frere Town, Mkomani, Ziwa la Ng’ombe na Kadzandani, yameandaliwa kwa lengo la kutoa jukwaa kwa vipaji vya vijana huku yakihamasisha mshikamano na maendeleo ya jamii.
Waandalizi wanasema kuwa mbali na ushindani wa soka, mashindano hayo yatatumika kama kampeni ya kuelimisha vijana kuhusu madhara ya matumizi ya dawa za kulevya, uhalifu pamoja na vitendo vya vurugu viwanjani maarufu kama hooliganism.

Aidha, mashindano hayo yanatarajiwa kuwaleta pamoja mamia ya vijana, viongozi wa jamii na wadau wa michezo, wakiamini kuwa soka lina nafasi kubwa katika kujenga mshikamano na kuhamasisha maendeleo ya kijamii.
Kaulimbiu ya mashindano hayo ni kujenga Nyali yenye umoja, amani na fursa kwa vijana kupitia michezo, huku waandaaji wakisisitiza kuwa ni wakati wa wakazi wa Nyali kushirikiana kujenga jamii bora kupitia vipaji vya michezo.

Mashindano ya Elkana Jacob Football Tournament, makala ya kwanza, yanatarajiwa kuwa moja ya matukio makubwa ya michezo ya jamii katika eneo la Nyali mwaka huu, huku wadau wakisubiri kwa hamu kipenga cha kuanza kwa michuano hiyo.
