
Serikali imesema imejipanga kuimarisha vita dhidi ya biashara haramu ya dawa za kulevya huku ikiongeza huduma za matibabu, ushauri nasaha na urekebishaji kwa waathirika ili warejee katika maisha ya kawaida.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Idara ya Usalama wa Ndani na Utawala wa Kitaifa, Dkt. Raymond Omollo, aliyemwakilisha Waziri Kipchumba Murkomen, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa Dhidi ya Matumizi Mabaya ya Dawa za Kulevya na Usafirishaji Haramu yaliyofanyika mjini Mombasa.

Kwa upande wake, Gavana wa Mombasa alieleza hatua zinazochukuliwa na serikali ya kaunti katika kukabiliana na athari za matumizi ya dawa za kulevya.

Naye Mbunge wa Jomvu Badi Twalib alitoa wito kwa jamii kushirikiana na vyombo vya usalama katika kukomesha usambazaji wa dawa za kulevya.

Seneta Maalum Miraj Abdillahi kwa upande wake alisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika elimu, ushauri nasaha na kuwawezesha vijana ili kuwaepusha na matumizi ya dawa za kulevya.
Maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na NACADA yaliwaleta pamoja viongozi wa serikali, Serikali ya Kaunti ya Mombasa, mashirika mbalimbali na wananchi, huku washiriki wakifanya maandamano ya amani kutoka Changamwe chini ya kaulimbiu “Support, Don’t Punish.”
