Majonzi Ndatani: Ndovu Waua Mtoto, Wakazi Walia Kukosa Haki na Ulinzi

Share this to

Wakazi katika eneo la Ndatani wametoa wito kwa serikali ya kitaifa na serikali ya kaunti ya Kilifi kujengewa uzio wa umeme kwa dharura kuzuia ndovu na wanyama wa porini wanaohangaisha maisha yao mara kwa mara.

Wakizungumza na waandishi wa habari katika Kaunti ya Kilifi wakazi hao aidha wametaka afisa wa wanyama pori kuongeza doria na kupewa fidia kwa hasara wanazopata .

Kwa mujibu wa wakazi hao janga hilo limeathiri maisha yao huku simulizi ya mzazi mmoja aliyempoteza mwanawe mwaka wa 2021 ikigusa nyoyo za wengi.

“Kwa miaka minne sasa sijapatiwa majibu yoyote kuhusu kifo cha mtoto wangu,” alisema mzazi huyo kwa uchungu, akionyesha hasira na kukata tamaa kwa ukimya wa mamlaka.

Mtoto wake alishambuliwa na ndovu karibu na boma lao, tukio lililobadili maisha ya familia hiyo milele. Hadi leo, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa kuwapa jibu au faraja.

Wakazi wengine nao wamesema kuwa maisha yao yamegeuka kuwa ya mateso baada ya mimea yao kuharibiwa huku watoto na akina mama wakiishi kwa hofu.

Wakazi wa eneo hilo wanahisi wamesahaulika na serikali, licha ya kupeleka malalamiko yao kwa maafisa wa Huduma ya Wanyamapori ya Kenya (KWS) mara kadhaa.

“Hatutaki kuendelea kuishi kwa hofu kila siku,” alisema mmoja wa wakazi kwa hasira. “Tumechoka kuomboleza, tumechoka kupoteza mali zetu na wapendwa wetu bila msaada wowote.”

Kufikia sasa KWS haijatoa tamko lolote rasmi kuhusu kisa hiki cha kusikitisha au hatua zinazopangwa kuchukuliwa. Wakazi wa Ndatani wameapa kutonyamaza hadi suluhu ipatikane.


Share this to

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *