Share this to

By:Hassan Pojjo

Juhudi za kukuza soka la wanawake katika Wadi ya Mwavumbo, Kaunti ya Kwale, zinaendelea kuzaa matunda baada ya timu ya South Calif Ladies ya Mkilo kufanikisha kwa mara ya kwanza ushiriki wa timu za wasichana kutoka eneo la Mwabila Cluster katika mashindano ya Chapa Dimba na Safaricom.

Hatua hiyo imeelezwa kuwa mafanikio makubwa yanayotokana na ushirikiano wa karibu kati ya makocha wa timu mbalimbali za wasichana katika Wadi ya Mwavumbo, ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa pamoja kuendeleza vipaji vya soka, kuhamasisha jamii kupinga dhuluma dhidi ya watoto wa kike na kusisitiza umuhimu wa elimu kwa wasichana.

Kwa mujibu wa mwanzilishi wa mpango huo, Timna Dzame, timu za wasichana katika eneo hilo zimekuwa zikikutana mara kwa mara kupitia mechi za kirafiki, hatua iliyochangia kuboresha kiwango cha mchezo, kuimarisha mshikamano na kuongeza kujiamini kwa wachezaji wanaposhiriki mashindano mbalimbali.

Kutokana na maandalizi hayo, South Calif Ladies imeendelea kufanya vizuri katika mechi za kirafiki, ikirekodi ushindi nyumbani na ugenini. Mafanikio hayo yameifanya timu hiyo kuwa mfano wa maendeleo ya soka la wanawake katika Wadi ya Mwavumbo.

Timna amesema lengo kuu la juhudi hizo ni kuunganisha nguvu za timu zote za mashinani ili hatimaye kusajili angalau timu moja ya wanawake katika mashindano yanayosimamiwa na Shirikisho la Soka Kenya (FKF), hatua itakayofungua fursa kwa wachezaji wengi kucheza katika viwango vya juu.

Amebainisha kuwa ndani ya miaka miwili tangu kuanzishwa kwa South Calif Ladies, timu hiyo imepiga hatua kubwa kutokana na nidhamu, kujituma kwa wachezaji na usimamizi mzuri wa benchi la ufundi.

Mafanikio hayo tayari yameanza kuonekana, ambapo mmoja wa wachezaji wa timu hiyo amefanikiwa kujiunga na Shule ya Upili ya Kwale High, jambo linalodhihirisha kuwa michezo inaweza kwenda sambamba na elimu.

Aidha, Timna amewahimiza wazazi kuwapa watoto wao wa kike nafasi ya kushiriki michezoni, akisisitiza kuwa ushirikiano kati ya wazazi na makocha ni msingi muhimu wa kukuza vipaji na kuwawezesha wasichana kutimiza ndoto zao.

“Licha ya changamoto za ukosefu wa vifaa vya mazoezi, tumekuwa tukihakikisha usalama wa wachezaji na kudumisha nidhamu uwanjani. Hayo ndiyo maadili yanayotuwezesha kuendelea kupiga hatua,” alisema.

Kwa sasa, Wadi ya Mwavumbo ina zaidi ya timu kumi za wasichana, huku eneo la Mwabila likiongoza kwa idadi ya timu, likifuatiwa na Kalalani.

Wadau wa michezo wanaamini kuwa ongezeko hilo linaashiria ukuaji wa soka la wanawake katika eneo hilo na linaweza kuwa chachu ya kuibua vipaji vitakavyoiwakilisha Kaunti ya Kwale na taifa katika siku zijazo.

Aidha, wamepongeza juhudi za South Calif Ladies na wadau wengine wakisema kuwa kuwekeza katika soka la wanawake kutasaidia kupunguza changamoto zinazowakabili wasichana, kuwapanulia fursa za elimu na maendeleo, pamoja na kuongeza ushiriki wao katika shughuli za kijamii na kiuchumi kupitia michezo.


Share this to

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *