By:Alii Vincent

Idara ya Usalama katika eneo bunge la Jomvu, Kaunti ya Mombasa, imetoa tahadhari dhidi ya ongezeko la makundi ya vijana wanaojikusanya na kuhangaisha wakazi wa maeneo mbalimbali.
Akizungumza katika mkutano uliofanyika katika Shule ya Badi Twalib, eneo la Aldina, Naibu Kamishna wa Kaunti wa Jomvu, Dolphine Okondo, alisema vijana watakaobainika wakijihusisha na vitendo vya uhalifu watakamatwa, kufikishwa mahakamani na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Wakati huo huo, Okondo amewataka wazee wa mitaa kuongeza juhudi katika kutekeleza majukumu yao, akibainisha kuwa serikali ya Rais William Ruto imeanza kuwapatia motisha kupitia mpango wa kiinua mgongo ili kuboresha utendaji wao.
Pia aliwahimiza wazee wa mitaa kushirikiana na viongozi wengine wa jamii kuhakikisha hakuna mtoto anayesalia nyumbani badala ya kuhudhuria masomo. Alisema watoto wanaokosa kwenda shule wako katika hatari kubwa ya kushawishiwa kujiunga na makundi ya uhalifu na kujihusisha na vitendo vinavyohatarisha usalama wa jamii.
