Share this to

By:Farida Ali

Ukurasa mpya wa uwezeshaji vijana umeanza kuandikwa jijini Mombasa, baada ya Serikali ya Kaunti kusajili zaidi ya taasisi 400 za mafunzo ya ufundi chini ya mpango wa Elimu Scheme – Skills Mtaani.

Mpango huo unalenga kusogeza mafunzo ya vitendo karibu na vijana katika mitaa mbalimbali, ili kuwapa nafasi ya kujifunza ujuzi unaoweza kuwawezesha kujiajiri na kupata ajira bila kulazimika kusafiri mbali kutafuta mafunzo.

Mafunzo hayo yanajumuisha ufundi wa umeme, ushonaji, urembo wa henna, uchomeleaji wa vyuma, TEHAMA na taaluma nyingine zinazohitajika katika soko la ajira na biashara.

Zaidi ya taasisi 400 zimesajiliwa chini ya mpango huo, hatua inayolenga kupanua wigo wa mafunzo ya ufundi na kuhakikisha vijana wengi zaidi, hasa wale wanaotoka katika maeneo yenye fursa chache, wanapata ujuzi wa kuwaongezea kipato.

Kwa mujibu wa serikali ya kaunti, mpango huo pia unalenga kukuza ujasiriamali miongoni mwa vijana, kuongeza ajira na kuwapa uwezo wa kuanzisha shughuli zao wenyewe za kiuchumi.

Chini ya kauli mbiu “Ujuzi Mtaani, Fursa Mtaani,” Skills Mtaani inalenga kuunganisha ujuzi na fursa, huku vijana wakipewa maarifa ya vitendo yanayoweza kutumika moja kwa moja katika maisha ya kila siku.

Akizungumza wakati wa usajili wa taasisi hizo, Gavana wa Mombasa amesema serikali ya kaunti imejitolea kuhakikisha kila kijana anapata fursa sawa ya kujifunza, kupata ujuzi na kujikwamua kiuchumi.

Amesema uwekezaji katika ujuzi wa vijana ni sehemu muhimu ya kujenga nguvu kazi yenye uwezo na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika Kaunti ya Mombasa.

Mpango huo unatarajiwa pia kuimarisha ushirikiano kati ya serikali ya kaunti, taasisi za mafunzo na sekta binafsi ili kuhakikisha vijana wanapata ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko.


Share this to

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *