
Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuongeza idadi ya watalii wanaozuru Kenya kutoka milioni 2.3 hadi kufikia milioni 5 ifikapo mwaka ujao.
Haya yamebainishwa na Katibu wa Wizara ya Utalii, Julius Bitok, wakati wa kongamano la kila mwaka la Kenya Association of Hotel Keepers and Caterers (KAHC) linalofanyika mjini Malindi, Kaunti ya Kilifi.

Kongamano hilo la siku tatu limewakutanisha viongozi wa sekta ya utalii, wawekezaji na watunga sera kujadili ukuaji endelevu wa utalii, matumizi ya teknolojia ya kidijitali, uongozi jumuishi pamoja na mikakati ya kuimarisha ushindani wa sekta hiyo nchini.
Bitok amesema serikali imejizatiti kuimarisha mazingira ya uwekezaji na kuboresha huduma za utalii ili kufanikisha lengo hilo la kuongeza idadi ya wageni wa kimataifa.
Akizungumzia taarifa kuhusu ugonjwa wa Ebola, Bitok amewataka wananchi na vyombo vya habari kuepuka kusambaza taarifa zisizo sahihi zinazoweza kuathiri taswira ya nchi, akisisitiza kuwa Kenya ni salama kwa watalii na wageni wote.
Kwa upande wake, Mbunge wa Malindi, Amina Mnyazi, amewahimiza wakazi wa Malindi na Wakenya kwa ujumla kudumisha amani ili kuendelea kuvutia watalii, hatua ambayo itachangia kuongeza nafasi za ajira na kukuza uchumi wa eneo hilo.
Akizungumzia upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Malindi na uboreshaji wa Barabara ya Salagate, Mnyazi amesema tayari amewasilisha hoja hizo kwa serikali kuu na kuwataka wakazi kuwa na subira wakati mipango ya utekelezaji ikiendelea.
