By:Robert Mutasi

Baraza la Makanisa Nchini Kenya (NCCK) Ukanda wa Mashariki ya Juu limeonya vikali wanasiasa dhidi ya kugeuza nyumba za ibada kuwa uwanja wa kampeni za kisiasa, likiahidi kulinda utakatifu wa kanisa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027.
Akizungumza Isiolo siku ya Jumatatu, Mwenyekiti wa NCCK Isiolo, Nathan Maingi, alisema kanisa halitaruhusu tena wanasiasa kutumia mimbari kuendeleza maslahi yao ya kisiasa, akisema kanisa lazima libaki kuwa mahali patakatifu pa maombi na ibada.
“Nachukua nafasi hii kutahadharisha wanasiasa na kanisa tutajaribu kuilinda hadhi ya kanisa. Sisi wachungaji tutahakikisha ya kwamba siasa haifanyiki katika kanisa,” Maingi alisema.
Alisema kuanzia sasa, mwanasiasa yeyote anayetaka kuhudhuria ibada kanisani atatakiwa kuja peke yake, bila kuhamasisha umati wa watu wa kumpigia kelele na makofi, na hataruhusiwa kufanya kampeni ndani ya kanisa.
“Wakitaka kuja kufanya kampeni katika kanisa tunawaambia mtu aje akiwa yeye peke yake aombe Mungu yule ambaye wengine wanaomba. Akimaliza kuomba Mungu aende apewe jukwaa nje ili tuweze kulinda utakatifu wa makanisa yetu,” alisema.
Maingi alisisitiza kuwa tabia ya wanasiasa kuvamia makanisa na msururu mkubwa wa watu ili kushawishi waumini na kutafuta makofi lazima ikome, akisisitiza kuwa siasa lazima ziwekwe mbali na madhabahu.
“Ili tuhakikishe ya kwamba siasa tumeziweka kando ya kanisa, kanisa ni mahali pa maombi tu, ni mahali tunakuja kumheshimu Mungu na tutahakikisha ya kwamba tumemheshimu Mungu kwa uwezo wetu wote. Kwa hivyo makanisa tuko na jukumu na tutalitekeleza jukumu hilo,” aliongeza.
Mwenyekiti huyo wa NCCK pia alituma ujumbe mkali kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), ambayo imepewa mamlaka kikatiba kuandaa uchaguzi huru na wa haki. Aliitaka tume hiyo kutekeleza wajibu wake na kuhakikisha kuna uaminifu katika mchakato wa uchaguzi.
“Tunatuma ujumbe mkali kwa IEBC kwa sababu hao ndio wamepewa nafasi hii na Katiba ya kwamba waandae uchaguzi ambao ni wa huru na haki,” Maingi alisema.
Aidha, alilaani mwenendo unaoongezeka wa vijana kutumiwa vibaya na wanasiasa na rushwa ya kununua kura, akionya kuwa maovu hayo yanadhoofisha demokrasia.
“Tumeona vijana wetu wanatumiwa vibaya na wanasiasa, mambo ya kununua kura kwa pesa ili umchague mtu huyu au yule mwingine. Jambo hilo tunalikataa, tunalikemea na tunatangaza ya kwamba watu wapewe uhuru wao wa kupiga kura mahali wanapofaa na yule mtu ambaye ako na uadilifu,” alisema, akiwataka Wakenya kuchagua viongozi wenye maadili na wanaowajibika.
Wakati huo huo, Mwakilishi wa Wanawake wa NCCK Ukanda wa Mashariki ya Juu, Jocylene Kagendo, alielezea masikitiko yake kuhusu unyonyaji wa vijana na viongozi wa kisiasa, akisema inawaumiza wazazi kuona watoto wao wakitumiwa vibaya.
“Kama mzazi wakati tunaona watoto wetu wanatumiwa vibaya na viongozi hiyo inatukera mioyoni mwetu, kwa sababu wakati watoto wanatumiwa vibaya ni kumaanisha ya kwamba nchi yetu ni nchi itakaa ikiwa haina amani mahali popote pale,” Kagendo alisema.
Alikumbusha wanasiasa kuwa wao pia ni wazazi na wanapaswa kuwa kielelezo cha kuigwa badala ya kuchochea vijana.
“Hawa wanaotumia watoto wetu ni wazazi, hata kama ni wanasiasa wajue ya kwamba wao ni wazazi, wajue ya kwamba wanaishi wakiambia vijana wetu ya kwamba wao ndio viongozi wa kesho. Na wasipokuwa kielelezo bora kwa watoto wetu, tunaona mambo ya kutumika vibaya yamekuwa mengi sana hasa katika kaunti zote,” alilalamika.
Viongozi hao wa NCCK walitaka amani, uadilifu na heshima kwa michakato ya kidemokrasia nchi inapoelekea kipindi kijacho cha uchaguzi.
