Share this to

By:Alii Vincent

Zaidi ya familia 200 katika kijiji cha Mkwakwani, eneo bunge la Msambweni, Kaunti ya Kwale, zimeanzisha mapambano ya kisheria kudai umiliki wa ardhi ya ekari 53 wanayodai ilinyakuliwa isivyo halali na mwekezaji binafsi, licha ya muda wa ukodishaji wake kuisha zaidi ya muongo mmoja uliopita.

Wakazi hao wanasema ardhi hiyo ilimaliza muda wa ukodishaji (lease) mwaka 2013 na, kwa mujibu wa sheria, ilipaswa kurejeshwa kwa jamii. Badala yake, wanadai ilihamishiwa kwa mwekezaji binafsi katika mazingira wanayoyataja kuwa yasiyoeleweka, hatua ambayo wameifananisha na kuendelezwa kwa ukoloni wa ardhi dhidi ya wenyeji.

Wakazi hao wameapa kutokubali kile wanachokitaja kuwa unyakuzi wa ardhi yao wakisisitiza kuwa eneo hilo ni muhimu kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo shule, vituo vya afya na miradi mingine ya kijamii itakayoinufaisha jamii ya Mkwakwani.

Wakili anayewawakilisha familia hizo, Salim Mwadumbo, amesema maandalizi ya kufungua kesi tayari yamekamilika baada ya kukusanywa kwa stakabadhi na nyaraka zote muhimu zinazohitajika mahakamani. Amesema hatua iliyobaki ni kuwasilisha shauri hilo ili mahakama iamue hatima ya umiliki wa ardhi hiyo.

Mwadumbo amewahimiza wakazi kuendelea kuwa watulivu na kuepuka vitendo vinavyoweza kuvuruga amani huku wakisubiri haki ipatikane kupitia mfumo wa sheria.

Wakati huo huo, juhudi za mwakilishi wa mwekezaji anayedai kumiliki ardhi hiyo kuthibitisha uhalali wa hati ya umiliki mbele ya wakazi hazikufanikiwa baada ya kushindwa kuhudhuria mkutano wa jamii uliokuwa umeandaliwa kujadili mzozo huo.


Share this to

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *