By:Hassan Pojjo

Mashindano ya soka ya Rashid Abdallah Super Cup yamepata msukumo mpya baada ya Magic Drinks Kenya kusaini mkataba wa udhamini wa kusaidia uendeshaji wa mashindano hayo na kukuza vipaji vya vijana katika ukanda wa Pwani.
Akizungumza baada ya hafla hiyo, mwanzilishi wa mashindano hayo, Rashid Abdallah, alisema udhamini huo utainua kiwango cha mashindano na kuwapa vijana fursa ya kuonyesha vipaji vyao hadi ngazi za kitaifa na kimataifa.
Kwa upande wake, Magic Drinks Kenya ilisema imeamua kuunga mkono mashindano hayo kwa kutambua mchango wa michezo katika kuunganisha jamii, kukuza nidhamu na kuwapa vijana matumaini kupitia soka.
Akihitimisha, Rashid Abdallah amewaalika wakazi wa Pwani na wadau wa soka kujitokeza kwa wingi kushuhudia mashindano hayo, akisisitiza lengo la kuyafanya kuwa jukwaa la kukuza vipaji vya soka.
Wakati huohuo, Mashindano ya Kitaifa ya Michezo ya Muhula wa Pili ya Shule za Sekondari (KSSSA Term 2 Ball Games) yatafanyika kuanzia Julai 31 hadi Agosti 6, 2026 katika MPESA Foundation Academy mjini Thika, huku timu 16 zikishiriki mashindano ya Rugby ya Wachezaji Saba (7s).
Tayari, ratiba ya makundi imetolewa. Kundi A linajumuisha Bokoli Boys, Nairobi School, Anjego na All Saints Embu, huku Kundi B likiwa na Butula Boys, Upper Hill, St. Anthony na Kamuiru Boys.
Katika Kundi C, Rugby Force, Njabini, Kirangari Mutige na Tononoka zitawania nafasi ya kutinga hatua ya mtoano, huku Kwale High ikikabiliana na Laiser Hill, Cardinal Otunga na Kitondo School katika Kundi D.
Mashindano hayo yanatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa na kutumika kama jukwaa la kuibua vipaji vya rugby, huku wadau wakisubiri kwa hamu kuanza kwa mechi za ufunguzi mjini Thika.
