By:Hassan Pojjo

Klabu ya KJS FC imeendelea kuonyesha kiwango bora katika mashindano ya soka ya kuwania Kombe la Frederick Muli yanayoendelea katika Wadi ya Nguutani, eneo la Mwingi West, Kaunti ya Kitui, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Kakululo Bullets.
Mchezo huo uliochezwa katika Uwanja wa Muthuzini uliwashuhudia mashabiki wakishuhudia kandanda la ushindani, huku timu zote zikionyesha juhudi kubwa kutafuta ushindi.
KJS FC inayofundishwa na Kocha Mlorozi, imeendelea kuvutia mashabiki kutokana na kiwango kizuri cha uchezaji, nidhamu na uwezo wa wachezaji wake kutengeneza nafasi za mabao.
Bao muhimu la ushindi lilifungwa na mshambuliaji Kaboy Jnr dakika ya 39 baada ya kumalizia krosi safi kutoka kwa kiungo Shadow Mbosyo. Ushirikiano mzuri kati ya Shadow, Benja na Matata uliisaidia KJS FC kutawala sehemu kubwa ya mchezo.
Ushindi huo umeifanya KJS FC kuendelea kuimarisha nafasi yake kama miongoni mwa timu zinazotarajiwa kufanya vizuri katika mashindano hayo.
Viongozi wa klabu hiyo wamesema lengo lao si kutwaa mataji pekee, bali pia kutumia mashindano hayo kulea na kukuza vipaji vya vijana watakaoweza kushiriki ligi za juu nchini na hata kimataifa.
Akizungumza kwa njia ya simu, kiungo wa timu hiyo Shadow Mbosyo, alisema changamoto kubwa inayowakabili ni ukosefu wa wadhamini wa kusaidia maendeleo ya wachezaji.
“Tuna vijana wengi wenye vipaji vikubwa ambao wanaweza kufika mbali wakipata mazingira mazuri ya kuendelezwa,” alisema Mbosyo.
Mashindano hayo yanafadhiliwa na Frederick Muli, ambaye amekuwa akihamasisha maendeleo ya michezo ya vijana katika eneo la Nguutani, akiamini soka ni nyenzo muhimu ya kukuza vipaji na kuleta mshikamano katika jamii.
Wakazi wa Nguutani wameendelea kujitokeza kwa wingi kushuhudia michezo hiyo, huku mashabiki wakitarajia kuona KJS FC ikiendelea na kiwango chake kizuri katika harakati za kuwania taji la Kombe la Frederick Muli.
